OIC yasema mgogoro wa Syria unahitaji suluhisho la kisiasa
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiisalmu (OIC) amesema njia pekee ya kuupatia ufumbuzi mgogoro wa Syria ni mazungumzo na mikakati ya kisiasa.
Yousef Ahmad Al-Othaimeen, Katibu Mkuu wa OIC ameyasema hayo katika mkutano na waandishi wa habari akiwa pamoja na Sartaj Aziz, Mshauri wa Mambo ya Nje wa Waziri Mkuu wa Pakistan na kufafanua kuwa, jumuiya hiyo kama mwakilishi wa Umma wa Kiislamu, inaunga mkono njia za amani katika kuutafutia ufumbuzi mzozo wa Syria.
Amebainisha kuwa, Uislamu ni dini ya amani na kwa njia yoyote ile haiungi wala haitounga mkono harakati za kigaidi zinazoshuhudiwa katika pembe mbalimbali ya dunia.
Katibu Mkuu wa OIC ameongeza kuwa, kueneza chuki na woga dhidi ya Uislamu na Waislamu ni aina fulani ya ugaidi; na ugaidi unafaa kulaaniwa na kupigwa vita kwa nguvu zote, kwa kuwa hauna mipaka ya kijografia, dini wala kabila.
Yousef Ahmad Al-Othaimeen, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiisalmu (OIC) ambaye yuko katika ziara ya siku tatu nchini Pakistan amesisitiza kuwa, kuna haja kwa nchi za Kiislamu kushirikiana na kuwa na mshikamano ili kwa pamoja ziweze kutafutia ufumbuzi changamoto zinazoukabili ulimwengu wa Kiislamu.