May 02, 2017 16:35 UTC
  • Watu 72 wauawa katika matukio ya ufyatuaji risasi nchini Marekani

Kituo cha takwimu za vitendo vya ukatili wa utumiaji silaha nchini Marekani kimetangaza kuwa watu 72 wameuliwa katika matukio ya ufyatuaji risasi yaliyotokea kwenye maeneo tofauti ya nchi hiyo.

Kituo hicho cha ukusanyaji taarifa za matukio ya ukatili wa utumiaji silaha moto nchini Marekani kimetangaza leo kuwa watu wasiopungua 72 wameuliwa na wengine 131 wamejeruhiwa  katika kipindi cha masaa 48 yaliyopita katika matukio 229 ya ufyatuaji risasi yaliyoripotiwa katika maeneo tofauti nchini humo.

Kwa mujibu wa ripoti ya kituo hicho, mengi ya matukio hayo ya ufyatuaji risasi yametokea katika majimbo ya Texas, Kentucky na Carolina Kaskazini.

Maelfu ya watu wanauawa na kujeruhiwa kila mwaka nchini Marekani kutokana na utumiaji silaha moto.

Silaha zinauzwa kama bidhaa ya kawaida nchini Marekani

Kwa mujibu wa takwimu rasmi, kiwango cha uhalifu na jinai nchini Marekani ni cha juu zaidi mara 20 kulinganisha nchi nyengine zilizoendelea.

Tangu ulipoanza mwaka uliopita wa 2016 hadi sasa, zaidi ya matukio 50,000 ya mashambulio ya ufyatuaji risasi yameripotiwa nchini Marekani ambapo watu wasiopungua 13,000 wameuliwa na wengine 27,000 wamejeruhiwa.

Licha ya ombi lililotolewa na makundi ya kutetea haki za kiraia nchini Marekani, serikali ya nchi hiyo hadi sasa imeshindwa kuweka sheria za kudhibiti uuzaji silaha kutokana na nguvu na ushawishi wa lobi ya watengezaji na wauzaji silaha nchini humo…/

 

Tags