Putin: Uhusiano na Palestina ni muhimu kwa Russia
Rais Vladimir Putin wa Russia ameonana na Mahmoud Abbas, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina na kusema kuwa, nchi yake inalipa umuhimu suala la kuimarisha uhusiano wake na Palestina.
Putin alisema hayo jana Alkhamisi wakati alipoonana na Mahmoud Abbas katika mji wa bandari wa Sochi wa nchini Russia na kuongeza kuwa, uhusiano wa Moscow na Palestina una historia ndefu. Amesema, hivi sasa pia uhusiano wa pande mbili ni mzuri na ni wa kuaminiana.
Rais wa Russia amegusia pia mazungumzo ya mapatano kati ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina na utawala wa Kizayuni wa Israel na kusema kuwa, Moscow inaunga mkono suala la kuundwa nchi huru ya Palestina kwa mujibu wa maazimio ya kimataifa.
Kwa upande wake, Mahmoud Abbas, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amesema kuwa, nafasi ya Vladimir Putin katika kuimarishwa uhusiano wa Russia na Palestina ni muhimu sana.
Amesema, mwaka huu uhusiano wa Palestina na Russia unatimiza miaka 135 na kwamba taifa la Palestina linajivunia uhusiano wake huo kwani tangu uhusiano wa pande hizo mbili ulipoanzishwa haujavunjika hata siku moja na daima wananchi wa Palestina wamekuwa wakiihesabu Russia kwamba ni muungaji mkono wao.
Amekumbusha kuwa, miongoni mwa uungaji mkono wa Moscow kwa Palestina ni suala la kuundwa nchi huru ya Palestina kwenye mipaka ya 1967 mji mkuu wake ukiwa ni Baytul Muqaddas na Russia imekuwa ikilisisitizia mara kwa mara jambo hilo.
Amesema, mgogoro wa Palestina hautoweza kutatuliwa bila ya kushirikishwa Russia. Ikumbukwe kuwa Palestina imekuwa na ubalozi wake mjini Moscow tangu mwaka 1989, wakati wa Shirikisho la Umoja wa Kisovieti.