Chama cha Leba cha UK kuitambua Palestina kikiingia madarakani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i29184-chama_cha_leba_cha_uk_kuitambua_palestina_kikiingia_madarakani
Chama cha Leba cha Uingereza kimesema kitaitambua Palestina iwapo kitaibuka mshindi katika uchaguzi wa Juni 8 nchini humo.
(last modified 2026-03-03T12:46:59+00:00 )
May 16, 2017 23:09 UTC
  • Chama cha Leba cha UK kuitambua Palestina kikiingia madarakani

Chama cha Leba cha Uingereza kimesema kitaitambua Palestina iwapo kitaibuka mshindi katika uchaguzi wa Juni 8 nchini humo.

Hayo yalisemwa na Jeremy Corbyn, kiongozi wa chama hicho akiwa mjini Bradford jana Jumanne na kuongeza kuwa, ni katika manifesto ya chama hicho kulitambua mara moja taifa la Palestina iwapo wataibuka na ushindi katika uchaguzi wa mapema ulioitishwa na Waziri Mkuu, Theresa May.

Inafaa kuashiria hapa kuwa uchaguzi mkuu ujao nchini Uingereza ulipasa kufanyika mwezi Mei mwaka 2020, lakini mwezi jana Theresa May aliitisha uchaguzi wa kabla ya wakati hapo tarehe 8 mwezi Juni mwaka huu. 

Corbyn akichangia mjadala bungeni

Corbyn amesema serikali yake itashinikiza kusitishwa mara moja mzingiro wa kibaguzi, ukaliaji wa mabavu wa ardhi za Palestina sambamba na kuendelezwa ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi katika ardhi za Palestina.

Kiongozi wa Chama cha Leba cha Uingereza amebainisha kuwa, serikali yake itashinikiza kupewa kipaumbele mazungumzo na majadiliano akisisitiza kuwa hatua za kijeshi haziwezi kuleta amani, usalama na uthabiti Mashariki ya Kati.

Kadhalika amesema iwapo atashinda katika uchaguzi huo, serikali yake itahakikisha kuwa migogoro inayoshuhudiwa hivi sasa katika nchi za  Libya, Nigeria, Sudan, Sudan Kusini, Somalia, Yemen na hata Kashmir, inapatiwa ufumbuzi kwa njia za kisiasa na kidiplomasia badala ya uingiliaji wa kijeshi.