HRW yakosoa muswada wa sheria dhidi ya wahamiaji Marekani
Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limekosoa vikali muswada uliopendekezwa na serikali ya Rais Donald Trump wa Marekani, ambao ukipasishwa na kuwa sheria basi vyombo vya dola vitaongezewa nguvu na mamlaka ya kuwabana zaidi wahamiaji haramu nchini humo.
Grace Meng, Mtafiti Mkuu wa shirika hilo amesema muswada huo hauna chochote kipya kinachoweza kupatia ufumbuzi kadhia ya wahajiri na unafanana na dikrii mbili zilizopasishwa na Trump huko nyuma dhidi ya wahamiaji ambazo mpaka sasa hazijakua na natija mbali na kupata pingamiza kutoka ndani na nje ya nchi.
Amesema muswada huo ni mwendelezo wa utawala wa Trump wa kuunda sera tata na zitakazokuwa na taathira hasi si tu kwa wahamiaji, bali pia kwa familia na jamii za Marekani.
Iwapo muswada huo unaotazamiwa kuidhinishwa hii leo na Kamati ya Mahakama ya Bunge utapasishwa na Kongresi ya Marekani, basi vyombo vya dola vitapewa mamlaka zaidi ya kufutilia mbali viza, kutumiwa nguvu kupita kiasi dhidi ya wahamiaji ambao hawajasajiliwa na serikali, kuwarejesha makwao kwa nguvu na kutolewa hukumu kali dhidi yao.
Mwezi Machi mwaka huu, Trump alipasisha agizo jipya la kibaguzi dhidi ya wahajiri kutoka nchi sita zenye idadi kubwa ya Waislamu ambazo ni Sudan, Somalia, Syria, Iran, Libya na Yemen, ambapo aliiondoa Iraq, iliyokuwa katika orodha ya awali ya nchi saba za Kiislamu ambazo raia na wakimbizi wake hawataruhusiwa kuingia nchini Marekani.
Zeid Ra’ad Zeid al-Hussein, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa alitangaza kuwa, amri hiyo ya Trump ya kuzuia raia wa nchi sita za Kiislamu kuingia nchini Marekani na hususan wakimbizi ni kinyume cha makubaliano na sheria za kimataifa, mbali na kuwabagua watu kwa misingi ya dini na imani zao za kiroho.