Marekani yakiri askari wake watatu wameangamizwa Afghanistan
Viongozi wa Marekani wametangaza kuwa askari watatu wa nchi hiyo wameuliwa na mwengine mmoja amejeruhiwa baada ya askari mmoja wa Afghanistan kuwafyatulia risasi wanajeshi wa Marekani huko mashariki mwa Afghanistan.
Msemaji wa kamandi ya jeshi la Marekani katika mji mkuu wa Afghanistan, Kabul amethibitisha kuuliwa askari hao wa Marekani na kueleza kwamba wanazo taarifa za tukio hilo lakini hawezi kulitolea ufafanuzi zaidi.
Hii ni katika hali ambayo msemaji wa Ikulu ya White House amesema Rais Donald Trump anafuatilia kwa makini matukio yanayojiri nchini Afghanistan ambako askari watatu wa nchi hiyo wameuawa.
Wakati huohuo msemaji wa kundi la Taliban Dhabihullah Mujahid ametangaza kuwa mwanachama wa kundi hilo ndiye aliyehusika na ufyatuaji risasi dhidi ya wanajeshi wa Marekani na kwamba katika shambulio hilo askari wanne waliuawa na wengine kadhaa walijeruhiwa.
Awali vyombo vya usalama vya Afghanistan vilitangaza kuwa wanajeshi wanne wa Marekani wameuawa katika mkoa wa Nangarhar mashariki mwa nchi hiyo.
Hivi sasa kuna wanajeshi wapatao 10,000 wa Marekani nchini Afghanistan.
Itakumbukwa kuwa mwaka 2001 Marekani iliivamia kijeshi Afghanistan kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi na kuyatokomeza makundi la Al-Qaeda na Taliban. Hata hivyo uvamizi na mashambulio ya kijeshi ya Marekani dhidi ya Afghanistan hayajawa na tija nyengine isipokuwa kusababisha raia zaidi ya elfu ishirini kuuawa na kuteketezwa miundombinu ya nchi hiyo.../