Marekani yatoa nyaraka za kuhusika kwake na mapinduzi ya Iran 1953
Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Marekani imetoa nyaraka zinazoonyesha kuwa, nchi hiyo ilihusika na njama za mapinduzi ya mwaka 1953 nchini Iran.
Mtandao wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Marekani umeonyesha nyaraka hizo zinazoeleza kwamba, Marekani ilihusika moja kwa moja katika mapinduzi yaliyoiondoa madarakani serikali ya wakati huo ya Muhammad Musaddiq nchini Iran.
Kwa mujibu wa nyaraka hizo ni kuwa, Washington ikiwa na lengo la kumuondoa madarakani Waziri Mkuu wa wakati huo wa Iran Dakta Mohammad Mosaddegh iliandaa mipango ya mapinduzi na kushiriki moja kwa moja katika mapinduzi hayo.
Licha ya kuwa, kabla ya hapo kumewahi kutolewa nyaraka zinazoonyesha kwamba, Marekani ilishiriki katika mapinduzi dhidi ya serikali ya Mohammad Mosaddegh mwaka 1953, lakini nyaraka za mara hii zina maelezo zaidi ikilinganishwa na za huko nyuma.
Shirika la Kijasusi la Marekani CIA kwa mara ya kwanza lilikiri mwaka 2013 kuhusika kwake katika kuipindua serikali iliyochaguliwa kidemokrasia Iran mwaka 1953.
Ikumbukwe kuwa mnamo Agosti 15 1953, mashirika ya kijasusi ya Marekani na Uingereza yalichochea mapinduzi yaliyotekelezwa na jeshi la Iran yaliyopelekea kuondolewa madarakani Mohammad Mosaddegh. Nchi hizo za Magharibi zilichochea mapinduzi hayo kufuatia hatua ya Mosaddegh ya kutaifisha sekta ya mafuta ya Iran ambayo wakati huo ilikuwa ikidhibitiwa na shirika la Uingereza.