Mtazamo wa G20 kwa bara la Afrika
https://parstoday.ir/sw/news/world-i31462-mtazamo_wa_g20_kwa_bara_la_afrika
Mkutano wa viongozi wa nchi wanachama wa G20 umeanza huko Hamburg nchini Ujerumani na miongoni mwa ajenda zake kuu ni mjadala juu ya mabadiliko ya hali ya hewa, mustakbali wa makubaliano ya kibiashara na matatizo na masuala ya bara la Afrika.
(last modified 2025-10-23T11:19:28+00:00 )
Jul 07, 2017 17:10 UTC

Mkutano wa viongozi wa nchi wanachama wa G20 umeanza huko Hamburg nchini Ujerumani na miongoni mwa ajenda zake kuu ni mjadala juu ya mabadiliko ya hali ya hewa, mustakbali wa makubaliano ya kibiashara na matatizo na masuala ya bara la Afrika.

Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel aliahidi katika mkutano wake uliofanyika siku kadhaa zilizopita na viongozi wa nchi kadhaa za Afrika kwamba, miongoni mwa mambo yatakayojadiliwa katika mkutano wa G20 ni jinsi ya kustawisha hali ya uchumi wa nchi za Afrika na kusaidia baadhi ya nchi za bara hiyo kuondoka katika migogoro. 

Japokuwa nchi za Magharibi siku zote zimekuwa zikiliangalia bara la Afrika kwa jicho la kikoloni lakini kutokana na mabadiliko ya kisiasa, kiuchumi na kiusalama yaliyotokea ulimwenguni na katika kanda hiyo, sasa Afrika imepata umuhimu mkubwa na makhsusi katika mfumo wa kimataifa; kwani kwa upande mmoja nchi za bara hilo zimekuwa medani ya ushindani mkubwa wa kiuchumi na kiusalama baina ya madola makubwa ikiwemo Marekani, Russia, China na Ulaya, na katika upande mwingine masuala kama ongezeko la wimbi la wahajiri haramu kutoka Afrika, ukame na njaa, na kushadidi harakati za makundi ya kigaidi na ya waasi na kupanuka zaidi harakati hizo hadi katika maeneo mengine ya dunia vimezidisha hamu ya nchi mbalimbali ya kutaka kuwepo katika bara hilo. Bangui

Rais wa Ufaransa akiwa safarini nchini Mali

Katika upande wa kiuchumi, Afrika imekuwa kivutio kikubwa cha vitega uchumi kutokana na utajiri wake wa maliasili na madini na nguvu kazi rahisi. Vilevile kuwa na jamii kubwa watu hususan ya vijana kunalifanya eneo hilo la Afrika kuwa soko lanalolengwa na nchi nyingi kubwa ukiwemo China. Harakati za kiuchumi na kibiashara zinazoongezeka kila uchao za China barani Afrika zinazitia wasiwasi na wahka mkubwa nchi za Magharibi hususan Marekani. Takwimu zinaonesha kuwa, biashara baina ya China ya Afrika imeongezeka zaidi ya mara ishirini tangu mwaka 2000. Mbali na masuala ya kiuchumi, China pia imezidisha ushawishi wake katika masuala ya kisiasa na kiusalama barani Afrika. Suala hilo limezidisha ushindani baina ya China na wakoloni wa zamani na wa sasa wa Magharibi kama vile Ufaransa na Marekani katika nchi za Afrika hususan katika sekta za nishati na madini.

Afrika ina umuhimu mkubwa pia katika masuala ya kisiasa na kiusalama. Baadhi ya madola makubwa ya Magharibi ikiweno Marekani yamejenga vituo na kambi za kijeshi katika nchi za Afika, na kuwepo kwa kambi hizo kunaziwezesha kudhibiti nchi za bara hilo na maeneo mengine. Hii ni pamoja na kuwa, vita na mapigano ya ndani katika baadhi ya nchi za Afrika vinalifanya bara hilo kuwa soko kubwa la kuuza silaha na zana za kivita kutoka nchi kubwa. Kwa sababu hiyo kunashuhudiwa ushindani mkubwa wa kutaka kudhibiti soko hilo.

Mapigano ya ndani katika nchi za Afrika yanatumiwa kama kisingizio cha kuwepo nchi za kigeni barani humo

Kushadidi harakati za kigaidi katika maeneo mbalimbali ya dunia likiwemo bara la Afika kumekuwa kisingizio kinachotumiwa na nchi za Magharibi kwa ajili ya kuimarisha uwepo wa nchi hizo katika nchi mbalimbali za eneo hilo chini ya mwavuli wa kupambana na ugaidi na wakati huo huo kudhamini malengo yao ya unyonyaji na ukoloni mamboleo.

Mtaalamu wa masuala ya Afrika na mwandishi wa kitabu cha "Wapenzi wa Afrika",  Hervé Bourges anasema: Hali ya kiuchumi ya Afrika na ongezeko la jamii ya watu wa bara hilo ni maudhui mbili muhimu ambazo haziwezi kupuuzwa kwa ajili ya mustakbali na siku zijazo. Anaongeza kuwa, kutokana na nafasi ya Afrika na umuhimu wake katika uwanja wa kimataifa, ni vigumu sana kuweza kulipuuza bara la Afrika. 

Sehemu ya mkutano wa G20, Ujerumani

Ni katika mazingira hayo ndipo viongozi wa G20 wanaoukutana Hamburg nchini Ujerumani wakaamua kujadili mauala mbalimbali yanayolihusu bara la Afrika.