Jul 20, 2017 14:04 UTC
  • UN: Ukimwi uliua watu milioni 1 mwaka 2016

Ugonjwa hatari wa ukimwi uliua watu milioni 1 mwaka uliopita wa 2016, ikiwa ni karibu nusu ya idadi ya watu walipoteza maisha kutokana na ugonjwa huo mwaka 2005 wakati wa kilele chake.

Kwa mujibu wa ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa, si tu kuwa vifo vinavyotokana na ugonjwa wa ukimwi au HIV/AIDS vimepungua bali pia watu wengi sasa wenye virusi hivyo wanapata matibabu ya kurefusha maisha.

Ripoti hiyo iliyochapishwa leo kabla ya mkutano wa Sayansi  na Ukimwi mjini Paris Jumapili imesema: "Mwaka 2016, watu milioni 19.5 kati ya milioni 36.7 wanaoishi na virusi vya HIV walikuwa wanapata matibabu."

Ripoti hiyo ya UNAIDS global roundup imesema: "Vifo vinavyotakana na Ukimwi vilipungua kutoka milioni 1.9 mwaka 2005 hadi milioni moja mwaka 2016."

Aidha ripoti hiyo imesema mwaka 2016 watu milioni 1.8 waliambukizwa Ukimwi katika hali ambayo mwaka 1997 ni watu milioni 3.5 ndio walioambukizwa ugonjwa huo. Kwa ujumla tokea muongo wa 1980 ni watu milioni 76.1 walioambukizwa Ukimwi duniani huku milioni 35 wakiaga dunia.

Daktari Peter Ghys kutoka UNAIDS Nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika zimekuwa msitari wa mbele katika kupunguza maambukizi kwa karibu asilimia 40 katika baadhi ya visa, lakini kwamba watoto na familia zisizojiweza zinasalia katika hatari.

 

Tags