Vijana 6 wa Burundi watoweka wakiwa Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i32106-vijana_6_wa_burundi_watoweka_wakiwa_marekani
Taarifa kutoka vyombo vya usalama nchini Marekani zinabaini kwamba vijana sita kutoka Burundi waliokuwa wakishiriki katika mashindano ya roboti nchini nchini humo wametoweka na hawajulikani waliko. Taarifa hizo hazijathibitishwa na serikali ya Burundi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 22, 2017 03:24 UTC
  • Vijana 6 wa Burundi watoweka wakiwa Marekani

Taarifa kutoka vyombo vya usalama nchini Marekani zinabaini kwamba vijana sita kutoka Burundi waliokuwa wakishiriki katika mashindano ya roboti nchini nchini humo wametoweka na hawajulikani waliko. Taarifa hizo hazijathibitishwa na serikali ya Burundi.

Waandalizi wa mashindano hayo wanasema kuwa waliwaeleza polisi baada ya msimamizi wa timu hiyo ya Burundi kushindwa kuwapata vijana hao.

Idara ya polisi mjini Washington imesema kuwa mara ya mwisho vijana hao kuonekana ilikuwa siku ya Jumanne wakati wa makamilisho ya michezo hiyo.

Vijana hao ambao ni wavulana wanne na wasichana 2 walio kati ya umri wa miaka 16 na 18 walipotea wakati wa mashindano hayo ya kwanza duniani yaliofanyika Washington DC.

Vijana hao wanatambulika kuwa Don Ingabire, Kevin Sambukiza, Nice Munezero, Audry Mwamikazi, Richard Irakoze na Aristide Irambona.

Kulingana na gazeti la The Washington Post, msemaji wa mashindano hayo Jose Escotto alisema, ripoti kamili imewasilishwa kwa polisi ambao wanachunguza kisa hicho.

Mashindano hayo yaliyohudhuriwa na timu 150 yanalenga kuwashawishi vijana kukuza vipaji vyao katika masomo ya sayansi, technolojia, uhandisi na hesabu.

Taarifa zaidi kutoka yombo vya usalama zinasema kuwa vijana wawili kati yao tayari wamevuka mpaka na kuingia nchini Canada.

Idara ya polisi ilibandika picha za sura za vijana hao sita waliopotea katika mtandao wao wa Twitter. Polisi imewataka raia kuwasiliana nao iwapo watakuwa na habari yoyote kuhusu vijana hao.