Onyo la Abdullah Abdullah kwa Marekani kufuatia mashambulizi yake nchini Afghanistan
Mkuu wa Baraza la Utekelezaji la Serikali ya Umoja wa Kitaifa nchini Afghanistan, Abdullah Abdullah amekosoa vikali mashambulizi ya jeshi la Marekani kwenye kambi za jeshi la serikali mkoani Helmand nchini humo.
Abdullah Abdullah ameionya Washington kutokariri tena mashambulizi ya namna hiyo nchini Afghanistan. Siku chache zilizopita ndege za kivita za Marekani zilifanya mashambulizi kwenye ngome za jeshi la serikali ya nchi hiyo katika eneo la Gereshk lililopo mkoa wa Helmand, ambapo makumi ya askari waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa. Hii sio mara ya kwanza ambapo jeshi la Marekani kwa kushirikiana na Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi (NATO) limefanya mashambulizi nchini Afghanistan na kusababisha mauaji ya halaiki dhidi ya askari na raia wa kawaida.
Mashambulizi ya jeshi la Marekani dhidi ya kambi za majeshi ya serikali yanayoendesha operesheni za kukabiliana na magaidi huko Syria na Iraq ni suala lililo wazi kwa mtu yeyote. Duru za kijeshi katika nchi hizo zimekuwa zikitangaza kwamba, wakati wowote ambapo jeshi la serikali linapopata ushindi dhidi ya magaidi, Marekani huwa inatekeleza mashambulizi ya kuwalenga askari hao wa serikali kwa lengo la kuwafanya magaidi waweze kukimbia kutoka uwanja wa mapigano na mzingiro wa askari wa serikali. Nchini Afghanistan pia katika siku za hivi karibuni askari wa serikali wamefanikiwa kupata ushindi mkubwa dhidi ya makundi ya kigaidi katika maeneo tofauti ya nchi hiyo. Ni kutokana na ushindi huo ndio maana jeshi la Marekani kama kamaida likazidisha operesheni ambazo kimsingi zinawalenga askari na raia wa kawaida wa nchi hiyo. Suala hilo limemfanya rais wa zamani wa Afghanistan, Hamid Karzai sambamba na kulaani hujuma hizo za jeshi la Marekani katika mkoa wa Helmand na Nangarhar akaitaja Washington kuwa muhusika mkuu wa kuendelea kwa machafuko, vitendo vya jinai na mgogoro nchini humo.
Ukweli ni kwamba, maisha ya askari na raia wa Afghanistan hayana thamani yoyote kwa Marekani na badala yake Washington inakusudia kuchochea harakati za kigaidi na kuendelea mgogoro nchini humo, kwani kuendelea kumwagika damu za Waafghanistani ni jambo ambalo halina umuhimu wowote kwa mvamizi huyo. Kufuatia hali hiyo Qazi Muhammad Hassan Hakiyar, mtaalamu wa masuala ya kisiasa anasema: "Katika siku za hivi karibuni raia wa Afghanistan si tu kwamba wamekuwa wahanga wa mashambulizi ya makundi ya kigaidi, bali pia wamekuwa wahanga na waathirika wakubwa wa hujuma za ndege za Marekani katika maeneo tofauti ya nchi hiyo. Wamarekani wapo nchini Afghanistan kwa lengo tu la kuchochea machafuko na uasi ili kwa njia hiyo waweze kuendelea kusalia katika nchi hiyo ya Asia kwa maslahi yao binafsi." Mwisho wa kunukuu. Marekani ambayo mwaka 2014, iliondoa askari wake wengi kutoka Afghanistan, hivi sasa kwa kisingizio cha kutoa masaada kwa jeshi la nchi hiyo na kukabiliana na ugaidi imeanza tena kuongeza askari wake nchini humo.
Hii ni katika hali ambayo katika kipindi chote cha miaka 16 ya kuikalia kwa mabavu nchi hiyo, Washington haijawahi kushiriki katika operesheni yoyote yenye lengo ka kumaliza ugaidi bali kinyume chake mara zote imekuwa ikihusika katika kuchochea moto wa vitendo vya kigaidi na machafuko zaidi ili kupata sababu ya kuzuia upinzani wa kutaka askari hao wa kigeni waondoke Afghanistan. Rahmatullah Bijan Pour, mtaalamu wa masuala ya kisiasa wa Afghanistan anasema: "Tangu makumi ya miaka huko nyuma, Marekani imekuwa ikifuatilia kupata eneo la kuweka majeshi yake Afghanistan. Hivyo ikiwa kuna mtu ambaye anadhani kwamba Wamarekani wapo nchini Afghanistan kwa ajili ya kuboresha hali ya mambo ya nchi hiyo, basi atakuwa amekosea sana." Mwisho wa kunukuu. Alaa kulli hali, raia wa Afghanistan wanataraji viongozi wa nchi yao hawataishia katika kutoa vitisho pekee dhidi ya Marekani, bali watashirikiana na bunge la nchi hiyo kwa ajili ya kuhitimisha jinai za askari Wamarekani walioko nchini humo.