Waafghani: Marekani ndiyo chanzo cha ongezeko la dawa za kulevya nchini
https://parstoday.ir/sw/news/world-i32888-waafghani_marekani_ndiyo_chanzo_cha_ongezeko_la_dawa_za_kulevya_nchini
Raia wa Afghanistan wameendelea kuitaja Marekani kwamba, ndio muhusika mkuu wa ongezeko la uzalishaji wa madawa ya kulevya nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 08, 2017 22:05 UTC
  • Waafghani: Marekani ndiyo chanzo cha ongezeko la dawa za kulevya nchini

Raia wa Afghanistan wameendelea kuitaja Marekani kwamba, ndio muhusika mkuu wa ongezeko la uzalishaji wa madawa ya kulevya nchini humo.

Waheed Muzhda mtaalamu wa masuala ya kisiasa wa Afghanistan na raia wa nchi hiyo amefanya mazungumzo na Redio Tehran na kusema kuwa, tangu Marekani kwa kushirikiana na washirika wake ilipolishambulia taifa hilo kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi na magendo ya madawa ya kulevya mwaka 2001, uzalishaji wa madawa hayo hatari ya kulevya umeongezeka maradufu.

Waheed Muzhda mtaalamu wa masuala ya kisiasa wa Afghanistan

Ameongeza kuwa, moja ya malengo ya Marekani ya kuendelea kuwepo nchini Afghanistan ni kuchochea uzalishaji zaidi wa madawa ya kulevya, kwani suala hilo litaifanya idadi ya waraibu wa dawa za kulevya kuongezeka siku hadi siku na kwamba hadi sasa zaidi ya raia wa taifa hilo wapatao milioni tatu na laki tano tayari wameshakumbwa na janga hilo thaqili. Kabla ya hapo pia, Mohammad Hanif Daneshyar, Msemaji wa Wizara ya Kupambana na Madawa ya Kulevya nchini Afghanistan alinukuliwa akisema kuwa, mkoa wa Helmand unashika nafasi ya kwanza katika uzalishaji wa madawa ya kulevya nchini humo. Jumapili iliyopita pia, Bi, Salamat Azimi, Waziri wa Kupambana na Madawa ya Kulevya nchini humo alitangaza bayana kwamba, madola ya Magharibi ikiwemo Marekani ndio wahusika wakuu wa ongezeko la uzalishaji wa madawa ya kulevya ndani ya taifa hilo.

Bi, Salamat Azimi, Waziri wa Kupambana na Madawa ya Kulevya nchini humo

Katika fremu hiyo, hivi karibuni serikali ya Afghanistan na ofisi inayoshughulikia makosa yanayohusiana na madawa ya kulevya ya Umoja wa Mataifa zilitoa ripoti kwamba, uzalishaji wa madawa ya kulevya nchini humo umeongezeka kwa asilimia 43 ikilinganishwa na mwaka jana 2016. Inafaa kuashiria kuwa, Afghanistan inajulikana kuwa mzalishaji mkubwa wa bidhaa hiyo nyeusi duniani ambapo kwa sasa karibu watu milioni tatu na laki sita ni waraibu wakubwa. Marekani na Uingereza ambazo ziliivamia nchi hiyo tangu miaka 15 iliyopita, zinatajwa kuwa wahusika wakuu wa ongezeko la uzalishaji wa madawa hayo ya kulevya.