Marekani yaua raia 16 katika hujuma ya anga Afghanistan
Kwa akali raia 16 wameuawa kufuatia shambulizi la anga la muungano wa kijeshi wa nchi za Magharibi unaoongozwa na Marekani nchini Afghanistan.
Kwa mujibu wa shirika la habari la TOLO, Marekani na waitifaki wake walifanya hujuma hiyo ya anga Alkhamisi usiku katika wilaya ya Haska Mina, mkoani Nangarhar, mashariki mwa nchi karibu na mpaka na Pakistan.
Msemaji wa Gavana wa mkoa wa Nangahar, Attaullah Khogyani amethibitisha kutokea shambulizi hilo ingawaje hajafafanua iwapo hujuma hiyo imefanywa na ndege za jeshi la Marekani au Shirika la Kijeshi la NATO lenye askari wapata elfu tano nchini Afghanistan.
Katika hali ambayo Marekani yenye wanajeshi 8,400 nchini Afghanistan imekuwa ikiihadaa jamii ya kimataifa kuwa inapambana na ugaidi nchini Afghanistan, duru mbalimbali za habari zimekuwa zikiripoti kuwa, Washington imekuwa ikiyapa silaha magege ya kigaidi nchini humo.
Mwezi uliopita, shirika la habari la Avay la Afghanistan lilimnukuu Maria Zakharova, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia akiwaambia waandishi wa habari kwamba, nchi yake ina taarifa mpya zinazoonesha kuwa kuna helikopta zisizojulikana zimetumika nchini Afghanistan kulisaidia genge la kigaidi la Daesh ikiwa ni pamoja na kuwahamisha wanachama wake kutoka sehemu moja hadi nyingine mashariki mwa Afghanistan na pia kuwatumia silaha na zana za kijeshi.
Hadi hivi sasa viongozi wa Afghanistan na maafisa wa shirika la kijeshi la NATO wameshindwa kusema chochote kuhusiana na matamshi hayo ya msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia.