Mamia ya Waislamu waandamana dhidi ya ugaidi nchini Uhispania
Mamia ya Waislamu katika mji wa Barcelona kaskazini mashariki mwa Uhispania wamefanya maandamano kulaani na kupinga mashambulizi mawili ya kigaidi yaliyotokea nchini humo siku chache zilizopita.
Waislamu hao jana Jumamosi waliandamana katikati mwa mji wa Barcelona wakipiga nara dhidi ya ugaidi na kusisitiza kwamba, Waislamu wako mbali kabisa na wanajitenga na watu uwenye misimamo ya kufurutu ada na wabaguzi.
Mandamano hayo yamefanyika baada ya polisi ya Uhispania juzi usiku kuzuia kufanyika maandamano ya wabuguzi wa Kihispania katikati mwa mji wa Barcelona.
Watu 14 waliuawa na wengine zaidi ya 100 kujeruhiwa katika shambulizi la kigaidi la Alkhamisi iliyopita huko Uhispania.
Shambulizi hilo lilifanyika baada ya gaidi kuwagonga kwa makusudi watu waliokuwa wakitembea kwa miguu katika eneo la kitalii la Las Ramblas katikati ya jiji la Barcelona na kukanyaga makumi ya watu.
Mapema juzi Ijumaa pia polisi ya Uhispania iliwapiga risasi na kuwaua watu watano wanaoshukiwa kuwa magaidi. Watu hao walijaribu kugonga watu waliokuwa wakitembea kwa miguu katika eneo la Cambrils lililoko umbali wa kilomita 120 kutoka Barcelona. Polisi wanasema washukiwa hao wamejeruhi raia 6 na polisi mmoja.