Wafuasi wa Jubilee waandamana Kenya kupinga uamuzi wa Mahakama
Polisi nchini Kenya wamelazimika kutumia gesi ya kutoa machozi kuwatawanya wafuasi wa chama cha Jubilee cha Rais Uhuru Kenyatta ambao walikuwa wakiandamana nje ya Mahakama ya Kilele mjini Nairobi wakipinga uamuzi wa mahakama hiyo kubatilisha uchaguzi wa rais wa Agosti 8.
Waandamanaji hao ambao agalabu yao walikuwa vijana, waliwatuhumu majaji wa mahakama hiyo kuwa walitoa uamuzi ulio kinyume cha sheria. Aidha wamesema mahakama hiyo ingepaswa kuamuru kura zihesabiwa upya badala ya kurudia uchaguzi kufuatia kesi iliyowalishwa na mgombea urais aliyeshindwa, Raila Odinga wa muungano wa NASA akipinga kutangazwa Uhuru Kenyatta kuwa mshindi katika uchaguzi huo.
Mahakama Kuu ya Kenya imesema kesho itachapisha uamuzi kamili wa kesi hiyo ambao ulitolewa Septemba Mosi. Uchaguzi wa marudio Kenya unatakiwa kufanyika siku 60 baada ya uamuzi huo na Tume Huru ya Uchaguzi (IEBC) imesema iko tayari kuandaa uchaguzi Oktoba 17 ingawa kuna tetesi kuwa, yumkini uchaguzi huo ukafanyika mwishoni mwa mwezi huo huo.
Waandamanaji ambao awali walijumuika katika Bustani ya Uhuru mjini Nairobi walikuwa wamebeba mabango yaliyokuwa yameandikwa "Maraga lazime aondoke" wakishinikiza kutimuliwa Jaji Mkuu wa Kenya, David Maraga aliyetangaza uamuzi huo.
Maandamano kama hayo pia yameshuhudiwa katika miji ya Nakuru na Naivasha ambayo ni kati ya ngome muhimu za Rais Kenyatta ambaye pamoja na kutangaza kukubali maamuzi ya mahakama aliwataja majaji wanne kati ya saba waliobatilisha uchaguzi wake ni wakora.
Wakati huo huo Jaji Mkuu wa Kenya Maraga amehutubia waandishi habari na kubainisha wasiwasi wake kufuatia maandamano hayo na hujuma dhidi ya majaji. Ameonya kuwa wenye kutoa matamshi ya kichochezi dhidi ya majaji ndio watakaobeba lawama iwapo lolote baya litakalowakumba majaji hao na familia zao.