Ofisi inayoshughulikia maslahi ya Iran nchini Marekani yashambuliwa
Ofisi inayoshughulikia maslahi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Washington imevamiwa, masaa machache baada ya hotuba ya kichochezi iliyotolewa na Rais Donald Trump wa Marekani, dhidi ya makubaliano ya nyuklia ya Iran.
Shirika rasmi la habari la Iran IRNA limeripoti kuwa, wavamizi wasiojulikana walishambulia ofisi hiyo ya kidiplomasia ya Iran kwa mawe na bunduki za upepo (air gun) jana Jumamosi.
Mkuu wa ofisi hiyo, Mehdi Atefat, amesema vioo vya ofisi hiyo vimefunjwa katika uvamizi huo, huku risasi zikitapakaa katika jengo hilo. Hata hivyo hakuna habari zozote za majeruhi zimeripotiwa katika tukio hilo.
Habari zaidi zinasema kuwa, kaulimbiu za chuki dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia zilikuwa zimeandikwa kwenye kuta za jengo hilo.
Ijumaa iliyopita, Trump aliituhumu tena Iran kuwa imekiuka makubaliano hayo ya nyuklia yanayojulikana kama JCPOA, licha ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA kuthibitisha mara nane kuwa Tehran imefungamana nayo.
Huku akitoa bwabwaja na matamshi yasiyo na msingi dhidi ya Iran, alisema kuwa makubaliano ya JCPOA ndiyo mabaya zaidi kuwahi kufikiwa katika historia ya Marekani na kwamba atahitimisha makubaliano hayo muda wowote atakapoona lazima kufanya hivyo.