Waliofariki dunia kwa kimbunga, mafuriko Vietnam wapindukia 70
https://parstoday.ir/sw/news/world-i35723-waliofariki_dunia_kwa_kimbunga_mafuriko_vietnam_wapindukia_70
Watu wasiopungua 72 wamepoteza maisha kufikia sasa kutokana na mafuriko na vimbunga katika maeneo ya kaskazini na katikati ya Vietnam.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Oct 16, 2017 08:07 UTC
  • Waliofariki dunia kwa kimbunga, mafuriko Vietnam wapindukia 70

Watu wasiopungua 72 wamepoteza maisha kufikia sasa kutokana na mafuriko na vimbunga katika maeneo ya kaskazini na katikati ya Vietnam.

Shirika la Kupambana na Majanga la nchi hiyo limewataka wakazi wa maeneo hayo wahame na kwenda nyanda za juu kuanzia leo Jumatatu ili kuepusha maafa zaidi.

Taarifa ya shirika hilo imesema maelfu ya nyumba katika maeneo hayo yamesombwa na mafuriko hayo, huku ekari 54 elfu ya mashamba ya mpunga yakiharibiwa na janga hilo.

Habari zinasema mafuriko hayo yaliyoanza tangu wiki iliyopita na kuharibu miundombinu yanahesabiwa kuwa makubwa zaidi katika miaka ya hivi karibuni.

Mafuriko nchini Vietnam

Watu karibu 20 wamefukiwa kwenye maporomoko ya udongo katika mkoa wa Hoa Binh ambao ni katika maeneo yaliyoathiriwa zaidi na majanga hayo ya kimaumbile.

Serikali imeonya kuwa, Kimbunga Khanun kinatazamiwa kusababisha mvua kubwa kuanzia leo Jumatatu katika maeneo ya kaskazini na katikati ya nchi hiyo ya Asia.

Imewataka wakazi wa maeneo hayo wanaotumia boti na mitumbwi kugura na kutoelekea sehemu inakotokea kimbunga hicho.