Trump alaaniwa katika kila kona ya dunia
https://parstoday.ir/sw/news/world-i37295-trump_alaaniwa_katika_kila_kona_ya_dunia
Uamuzi wa rais wa Marekani wa kuutangaza mji mtakatifu wa Quds wenye Kibla cha Kwanza cha Waislamu kuwa eti ni mji mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel umeendelea kulaaniwa na hata waitifaki wa karibu wa Marekani katika kila kona ya dunia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 07, 2017 04:07 UTC
  • Trump alaaniwa katika kila kona ya dunia

Uamuzi wa rais wa Marekani wa kuutangaza mji mtakatifu wa Quds wenye Kibla cha Kwanza cha Waislamu kuwa eti ni mji mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel umeendelea kulaaniwa na hata waitifaki wa karibu wa Marekani katika kila kona ya dunia.

Nchi za Ulaya ikiwemo Uingereza ambayo ni muitifaki wa karibu zaidi wa Marekani, zimelaani uamuzi huo wa Trump na kusema unalenga kuchochea machafuko. Hata Papa Francis, kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani amemlaumu Trump kwa uamuzi wake huo usio wa kimantiki.

Katika hotuba yake ya jana Jumatano, Donald Trump alidai kuwa, suala la kuitangaza Quds kuwa mji mkuu wa utawala wa Kizayuni ilibidi lifanyike miaka mingi nyuma na kwamba serikali yake imechukua uamuzi huo ambao umewashinda marais wote waliotangulia wa Marekani.

Askari makatili wa Israel wakivamia maeneo matakatifu ya Waislamu huko Quds

 

Aidha ametoa amri ya kuanza mchakato wa kuuhamishia Quds, ubalozi wa Marekani ulioko Tel-Aviv, mji mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kupitia wizara yake ya mambo ya nje imelaani vikali hatua hiyo ya Trump na imetoa taarifa maalumu ikisisitiza kwamba tangazo hilo lilotolewa na Donald Trump ni ukiukaji wa wazi wa maazimio ya kimataifa. Viongozi mbalimbali wa Iran wanaendelea kulaani uamuzi huo.

Kabla ya hapo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei alikuwa amesema kuwa, Marekani, utawala haramu wa Israel na watawala wenye fikra mgando na wategemezi ni mafirauni wa zama hizi na kwamba, baadhi ya wanasiasa wa Marekani wametangaza waziwazi kuwa, lazima kutokee vita na machafuko magharibi mwa Asia (Mashariki ya Kati) ili utawala ghasibu wa Israel uwe katika amani na wakati huo huo kutapakaza damu katika ulimwengu wa Kiislamu na kuukwamisha usipate maendeleo.

Huko Palestina kwenyewe maandamano yanaendelea katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, Ghaza na nchi kama Jordan na Lebanon kulalamikia uamuzi wa rais wa Marekani ya kuitangaza Baytul Muqaddas kuwa eti ni mji mkuu wa Israel.