The Independent: Bin Salman ndiye 'shakhsia wa mwaka' kwa mapungufu
https://parstoday.ir/sw/news/world-i37711-the_independent_bin_salman_ndiye_'shakhsia_wa_mwaka'_kwa_mapungufu
Mwandishi mashuhuri wa habari wa gazeti la The Independent la Uingereza kwa njia ya kinaya amemuarifisha Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman kuwa 'shakhsia wa mwaka' kutokana na kufeli sera zake katika eneo la Mashariki ya Kati.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Dec 17, 2017 08:05 UTC
  • The Independent: Bin Salman ndiye 'shakhsia wa mwaka' kwa mapungufu

Mwandishi mashuhuri wa habari wa gazeti la The Independent la Uingereza kwa njia ya kinaya amemuarifisha Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman kuwa 'shakhsia wa mwaka' kutokana na kufeli sera zake katika eneo la Mashariki ya Kati.

Patrick Cockburn ameandika katika makala yake kwenye gazeti hilo kuwa, "Salman amevuna kinyume kabisa na matarajio ya sera zake za mambo ya nje haswa Mashariki ya Kati."

Mwandishi huyo mtajika wa Uingereza ameainisha namna mikakati ya Bin Salman imefeli, kuanzia kwa kile alichokitaja kama wimbi la vita dhidi ya ufisadi na kumshurutisha Waziri Mkuu wa Lebanon, Saad Hariri kujiuzulu.

Ameandika kuwa Bin Salman anatumia udikteta kuhakikisha kuwa anaandaa mazingira ya kumrithi babake.

Gazeti la Independent la Uingereza

Patrick Cockburn amebainisha kwa kuandika: "Mrithi huyo wa kiti cha ufalme anaamini kuwa njia ya pekee inayoweza kumfikisha katika kuhodhi madaraka kikamilifu nchini Saudia ni kushadidisha ukandamizaji, utiaji mbaroni watu na kuchukua hatua za kimaonyesho tu."

Itakumbukwa kuwa, Saudia ilimlazimisha Waziri Mkuu wa Lebanon kujiuzulu akiwa katika ardhi ya utawala huo wa kifalme, kwa kuibua tuhuma zisizo na msingi dhidi ya Iran. Hata hivyo Saad Hariri aliporejea nchini Lebanon alifutilia mbali mpango huo wa kujiuzulu.