Dec 28, 2017 08:02 UTC
  • 40 wauawa katika shambulizi la kigaidi Kabul, Afghanistan

Kwa akali watu 40 wameuwa na wengine 30 kujeruhiwa katika shambulizi la kigaidi lililoutikisa mji mkuu wa Afghanistan, Kabul.

Ismail Kawosi, msemaji wa Wizara ya Afya ya Umma wa nchi hiyo amethibitisha kutokea hujuma hiyo, ambapo mripuko mkubwa umesikika karibu na ofisi za shirika la habari la Afghan Voice News.

Mashuhuda wanasema miongoni mwa waliopoteza maisha katika shambulio hilo la leo ni wanafunzi, ambao walikuwa katika kikao cha mazungumzo na watafiti wa shirika hilo.

Mripuko wa Kabul

Naye Najib Danish, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani wa nchi hiyo ameutaja mlipuko huo kama shambulizi la kujitoa muhanga na kuongeza kuwa yumkini idadi ya wahanga wa hujuma hiyo ikaongezeka. Hadi tunanda mitamboni, hakuna kundi lililokuwa limedai kuhusika na shambulizi hilo la kinyama.

Wakati huo huo, wanafunzi sita wa shule ya chekechekea wameuawa baada ya gari walimokuwa wakisafiria kukanyaga bomu la kutegwa ardhini katika mkoa wa  Balkh nchini Afghanistan.

Tags