UNICEF yataka kuandaliwa mazingira ya kurejea wakimbizi watoto wa Myanmar
https://parstoday.ir/sw/news/world-i39457-unicef_yataka_kuandaliwa_mazingira_ya_kurejea_wakimbizi_watoto_wa_myanmar
Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa umetoa wito wa kuboreshwa mazingira ya kiusalama na kuandaliwa uwanja wa kurejea nchini Myanmar wakimbizi watoto wa Kiislamu wa jamii ya Rohingya walioko nchini Bangladesh.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jan 25, 2018 07:24 UTC
  • UNICEF yataka kuandaliwa mazingira ya kurejea wakimbizi watoto wa Myanmar

Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa umetoa wito wa kuboreshwa mazingira ya kiusalama na kuandaliwa uwanja wa kurejea nchini Myanmar wakimbizi watoto wa Kiislamu wa jamii ya Rohingya walioko nchini Bangladesh.

Justin Forsyth, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF amesema kuwa, asimilia 58 ya wakimbizi Waislamu wa Rohingya ni watoto na kwamba, akthari yao wameathirika pakubwa kutokana na vitendo vya utumiaji mabavu walivyovishuhudia kwa macho yao.

Akizungumza wakati alipotembelea kambi ya wakimbizi Waislamu wa jamii ya Rohingya wa Myanmar kusini mashariki mwa Dhaka mji mkuu wa Bangladesh, afisa huyo wa Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF amesisitiza kwamba, kurejea makwao wakimbizi hao kunapaswa kuwa ni kwa hiari na zoezi hilo lifanyike kwa usalama na kwa kuheshimiwa haki za wakimbizi hao.

Hayo yanaripotiwa katika hali ambayo, Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR linasema kwamba, hali katika mkoa wa Rakhine nchini Myanmar sio shwari kuweza kuwapokea malaki ya wakimbizi Waislamu wa jamii ya Rohingya waliokimbilia nchini Bangladesh.

Waislamu wa Myanmar wakikimbia makazi yao

Wakati huo huo, serikali ya Bangladesh imetangaza kuwa, wakimbizi Waislamu Warohingya waliopata hifadhi nchini humo kufuatia ukatili wanaotendewa nchini Myanmar, sasa wamefika milioni moja na idadi hiyo ni kubwa zaidi ya ile ambayo imekuwa ikitajwa katika vyombo vya habari.

Maelfu ya Waislamu wa kabila la Rohingya nchini Myanmar wameuawa na maelfu ya wengine kujeruhiwa tangu kuanza wimbi jipya la mashambulizi ya jeshi na Mabudha wenye misimamo mikali katika mkoa wa Rakhine magharibi mwa nchi hiyo tarehe 25 Agosti mwaka jana hadi sasa.