Netanyahu afuta makubaliano na UN kuhusu wahajiri wa Kiafrika
Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel amebatilisha makubaliano kati ya Tel Aviv na Umoja wa Mataifa, kuhusu kupelekwa katika nchi za Magharibi wahajiri wa Kiafrika wanaoishi katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala huo ghasibu.
Kufuatia mashinikizo ya wanasiasa wa mrengo wa kulia, Benjamin Netanyahu ametangaza kufutilia mbali makubaliano hayo yaliyofikiwa Jumatatu kati ya Israel na Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR, juu ya kupelekwa kwa wahajiri hao wa Kiafrika wapatao 39,000 katika nchi za Magharibi katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Mwezi Januari Utawala wa Kizayuni wa Israel ulianza kutekeleza mpango wa kuwatimua maelfu ya wahajiri hao wa Kiafrika walioingia katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala huo haramu.
Israel ilidai kuwa imeafikiana na Rwanda na Uganda juu ya kuwakabidhi wahajiri hao kwa nchi hizo, jambo ambalo lilipingwa vikali na viongozi wa nchi mbili hizo za Kiafrika, mbali na kukosolewa na watetezi wa haki za binadamu.
Aghalabu ya wahajiri hao wa Kiafrika ni raia wa Eritrea na Sudan.