Futari ya kimaonyesho ya Trump yakabiliwa na maandamano
https://parstoday.ir/sw/news/world-i45530-futari_ya_kimaonyesho_ya_trump_yakabiliwa_na_maandamano
Sambamba na kufanyika karamu ya futari iliyoiandaliwa na Rais Donald Trump wa Marekani, wanaharakati wa masuala ya kiraia wamefanya maandamano mbele ya Ikulu ya White House wakipinga siasa za chuki na ubaguzi za rais huyo dhidi ya Waislamu na wahajiri.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 07, 2018 03:39 UTC
  • Futari ya kimaonyesho ya Trump yakabiliwa na maandamano

Sambamba na kufanyika karamu ya futari iliyoiandaliwa na Rais Donald Trump wa Marekani, wanaharakati wa masuala ya kiraia wamefanya maandamano mbele ya Ikulu ya White House wakipinga siasa za chuki na ubaguzi za rais huyo dhidi ya Waislamu na wahajiri.

Waandamanaji hao walipiga nara dhidi ya njama za Trump katika kuwapiga marufuku raia wa nchi kadhaa za Kiislamu kuingia Marekani sambamba na kuitaja hatua hiyo kuwa ya chuki na ya kibaguzi. Futari ya Rais Donald Trump wa Marekani ilifanyika Jumatano ya jana katika Ikulu ya White House. Trump ambaye mara nyingi amekuwa akitoa matamshi ya chuki dhidi ya Waislamu alidai jana kwamba, hatua yake ya kutoitisha futari katika Ikulu ya White House katika mwaka wake wa kwanza wa urais, haikumaanisha kufumbia macho suna hiyo. Katika marasimu hayo ya futari ya jana zaidi ya wageni 50 walialikwa.

Waislamu na watetezi wa haki za binaadamu wakiandamana mbele ya Ikulu ya Marekani kulaani chuki za Trump dhidi ya Waislamu

Katika futari hiyo ya kimaonyesho, Trump alikaa meza moja na Khalid bin Salman bin Abdulaziz Al Saud, mtoto wa Mfalme wa sasa wa Saudia na ambaye pia ni balozi wa Saudia nchini Marekani kadhalika Dina Kawar, balozi wa Jordan nchini Marekani. Hii ni katika hali ambayo viongozi wa taasisi kubwa za Kiislamu nchini Marekani ikiwemo 'Jumuiya ya Kiislamu ya Amerika ya Kaskazini' na ambayo ni taasisi kongwe na kubwa zaidi ya Kiislamu nchini humo, zilisusia futari hiyo ya Trump. Kabla ya futari hiyo Colin Christopher mmoja wa viongozi wa ngazi za juu wa Jumuiya ya Kiislamu ya Amerika ya Kaskazini alituma barua pepe kwenda gazeti la Huffington Post la nchini Marekani akibainisha kwamba White House ilikuwa inapanga kuwaalika mabalozi wa nchi za kifisadi na ambazo zinakiuka haki za raia wake na Waislamu kushiriki futari hiyo.