Jul 18, 2018 02:31 UTC
  • Saudia yashitakiwa UN kwa kuingiza siasa katika ibada ya Hija

Kamati ya Kimataifa ya Kusimamia Haram Mbili za Makka na Madina imewasilisha barua mbili tofauti kwa Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa na Kamisheni ya Kidini na Uhuru wa Kujieleza ya Kamisheni ya Haki za Binadamu ya Bunge la Ulaya, ikiishitaki Saudi Arabia kwa kuingiza masuala ya siasa katika ibada ya Hija sambamba na kuweka mipaka ya uhuru wa kidini.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kamati hiyo imeeleza wasiwasi wake mkubwa kuhusu ongezeko la vitendo vya ukiukwaji wa haki za kidini na ibada ya Hija vinavyofanywa na Saudia na kusema kuwa, Riyadh inaendelea kuwakamata mahujaji na wafanya ibada ya Umrah baada ya kuwa wamekamilisha taratibu zote za kuingia nchini humo kwa ajili ya kutekeleza ibada. Taarifa hiyo imeongeza kwamba idadi kubwa ya Waislamu kwa sababu tu ya kuwa na itikadi tofauti au kwa sababu ya mataifa yao kuwa na tofauti za kisiasa na Saudia, wanatiwa nguvuni wanapoingia nchini humo kwa ajili ya kutekeleza ibada ya Hija.

Ibada ya Hija ambayo sasa inatumiwa kisiasa na Saudi kwa ajili ya kufikia malengo yake machafu

Kamati hiyo imetoa mfano wa masharti yaliyotangazwa na Saudia kwa ajili ya wafanya ibada ya Umra na Hija wa Qatar, kuwa ni aina fulani ya kiburi cha kisiasa na kwa ajili hiyo imetaka kulipwa fidia raia wa Qatar kutokana na hasara waliyoipata kutoka kwa serikali ya Riyadh baada ya kuzuiliwa kuingia nchini humo kutekeleza ibada.

Hivi karibuni Wizara ya Hija na Umra ya Saudia imetoa taarifa maalumu kuhusu masharti kwa raia wa Qatar wanaotaka kuhiji Hija ndogo ya Umra kwa kutangaza kuwa, raia wa nchi hiyo wanaoruhusiwa kwenda kufanya Umra mwaka huu ni wale tu watakaosafiri kutokea nje ya Qatar na kuingia Saudi Arabia kwa njia ya anga kupitia uwanja wa ndege wa Mfalme Khalid. Kufuatia masharti hayo Kamisheni ya Kitaifa ya Haki za Binadamu nchini Qatar imetangaza kwamba serikali ya Doha imewasilisha mashtaka yake katika Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu kufuatia kitendo cha Saudia kutumia siasa ndani ya ibada hiyo.

Tags