Afrika Kusini inaendelea kuziuzia Saudia, Imarati silaha zinazoua Wayemen
https://parstoday.ir/sw/news/world-i47051-afrika_kusini_inaendelea_kuziuzia_saudia_imarati_silaha_zinazoua_wayemen
Ripoti ya kila mwaka ya Kamati ya Kitaifa ya Kudhibiti Silaha nchini Afrika Kusini (NCACC) inaonesha kuwa, Saudi Arabia na Imarati zinaendelea kurundika silaha zinazonunua kutoka nchi hiyo ya Kiafrika, na ambazo zinatumika mashambulizi dhidi ya wananchi wa Yemen.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 27, 2018 03:21 UTC
  • Afrika Kusini inaendelea kuziuzia Saudia, Imarati silaha zinazoua Wayemen

Ripoti ya kila mwaka ya Kamati ya Kitaifa ya Kudhibiti Silaha nchini Afrika Kusini (NCACC) inaonesha kuwa, Saudi Arabia na Imarati zinaendelea kurundika silaha zinazonunua kutoka nchi hiyo ya Kiafrika, na ambazo zinatumika mashambulizi dhidi ya wananchi wa Yemen.

Tovuti ya Middle East Eye imeripoti kuwa, Afrika Kusini imeongeza kiwango cha silaha za kijeshi inazoziuzia Saudia na Imarati, na kwamba katika kipindi cha mwaka 2016 na mwaka jana 2017, nchi hiyo iliziuzia nchi hizo za Kiarabu zinazofanya mauaji Yemen silaha mbalimbali zikiwemo bunduki, magari ya kijeshi, mabomu ya mota, mfumo wa kisasa wa kamera za siri, teknolojia ya kijeshi na kadhalika, kwa thamani ya Rand bilioni 3 (dola milioni 228).

Licha ya wasiwasi mkubwa wa mashirika ya kutetea haki za binadamu kuhusiana hali mbaya ya kibinadamu Yemen, lakini Afrika Kusini na nchi kadhaa za Magharibi zimeendelea kuziuzia Saudia na Imarati silaha ambazo zinatumika katika hujuma dhidi ya wananchi wa Yemen. 

Mwezi huu Rais Cyril Ramaphosa  wa Afrika Kusini alizitembelea Saudia na Umoja wa Falme za Kiarabu na kusaini makubaliano ya kuimarisha uwekezaji ya dola bilioni 20 kutoka nchi mbili hizo.

Hali ya kibinadamu Yemen

Mwezi Machi mwaka 2015, na kwa msaada na uungaji mkono wa Marekani, Imarati na nchi nyingine kadhaa, Saudi Arabia ilianzisha uvamizi wa kijeshi dhidi ya Yemen sambamba na kuiwekea nchi hiyo mzingiro wa ardhini, angani na baharini.

Moto wa vita uliowashwa na Saudia na waitifaki wake nchini Yemen, hadi sasa umeteketeza roho za Wayemeni zaidi ya 14,000, umewajeruhi makumi ya maelfu na kusababisha mamilioni ya wengine kubaki bila makazi.