Hata Uingereza yapinga siasa za Trump dhidi ya Iran
https://parstoday.ir/sw/news/world-i47461-hata_uingereza_yapinga_siasa_za_trump_dhidi_ya_iran
Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza imesisitiza kuwa London itaendelea kuheshimu ahadi zake katika mapatano ya nyuklia na Iran maarufu kwa jina la JCPOA ni imekataa ombi la Marekani la kushirikiana nayo kuiwekea vikwazo Tehran.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 15, 2018 09:30 UTC
  • Hata Uingereza yapinga siasa za Trump dhidi ya Iran

Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza imesisitiza kuwa London itaendelea kuheshimu ahadi zake katika mapatano ya nyuklia na Iran maarufu kwa jina la JCPOA ni imekataa ombi la Marekani la kushirikiana nayo kuiwekea vikwazo Tehran.

Woody Johnson, balozi wa Marekani mjini London alikuwa ameiomba Uingereza ishirikiane na nchi yake kujitoa katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA na kuiwekea vikwazo Iran, lakini wizara ya mambo ya nje ya Uingereza imesema leo kuwa, London haiwezi kujitoa katika mapatano hayo na itaheshimu ahadi zake.

Wizara ya mambo ya nje ya Uingereza vile vile imesema, nchi hiyo ina nia ya kuruhusu mashirika yake yaendelee kushirikiana na Iran na yasiogopeshwe na vikwazo vya upande mmoja vya Marekani.

Rais wa Marekani, Donald Trump

 

Msimamo huo wa Uingereza ndio msimamo wa nchi zote wanachama wa Umoja wa Ulaya, na Woody Johnson, balozi wa Marekani mjini London alikuwa ameitaka nchi hiyo kuachana na msimamo wa Umoja wa Ulaya kuhusu mapatano ya nyuklia ya JCPOA. 

Itakumbukwa kuwa tarehe 8 Mei mwaka huu, rais wa Marekani, Donald Trump alitangaza kuitoa nchi yake katika mapatano ya kimataifa ya nyuklia licha ya kwamba Washington ilikuwa mstari wa mbele kufanikisha kufikiwa kwake. Baada ya kujitoa, Trump alirejesha vikwazo vilivyokuwa vimeondolewa dhidi ya Iran na kuzitaka nchi zote duniani zifuate amri yake vinginevyo ataziwekea vikwazo.

Hata hivyo msimamo huo wa Trump umegonga mwamba, kwani hata waitifaki wa karibu kabisa wa Marekani kama vile Uingereza wametangaza wazi kuwa hawatojitoa katika mapatano hayo ya JCPOA na hawatoshirikiana na Washington kuiwekea vikwazo vipya Iran.