Kuchaguliwa Imran Khan kuwa Waziri Mkuu mpya wa Pakistan
Kwa kupata kura 176 za wabunge wa bunge la taifa la Pakistan, Imran Khan, Mkuu wa Chama cha Tehreek-e-Insaf cha Pakistan ametangazwa kuwa Waziri Mkuu wa 22 wa nchi hiyo.
Baada ya kuchaguliwa, Khan aliapishwa katika ikulu ya nchi hiyo siku ya Jumamosi. Imran Khan anaanza kipindi cha uongozi nchini Pakistan katika hali ambayo nchi hiyo inapitia matukio muhimu katika historia yake. Kwa miaka kadhaa na baada ya nchi hiyo kupata uhuru, yaani mwaka 1947 viongozi na shakhsia kutoka vyama viwili vya Muslim League cha Nawaz Sharif na cha 'Wananchi' ndio wamekuwa wakiongoza nchi hiyo kwa kushikilia nafasi ya Waziri Mkuu na hata wakati jeshi lilipofanya mapinduzi, ni makamanda wa jeshi ndio waliotwaa nyadhifa za uongozi. Kwa mtazamo wa duru za kisiasa za nchi hiyo, hatua ya Imran Khan kuapishwa kuwa Waziri Mkuu wa Pakistan si tu kwamba inahesabiwa kuwa ya kipekee katika historia ya kisiasa ya nchi hiyo, bali inaakisi pia matakwa ya wananchi waliosema 'hapana' kwa mfumo wa kiutawala wa vyama viwili kwa ajili ya mabadiliko ya kina katika sekta tofauti za kisiasa, kiuchumi na kijamii nchini humo.
Matarajio ya Imran Khan kwamba anaweza kuyafikia malengo yake ya kisiasa, kiuchumi na kijamii nchini Pakistan katika kipindi kifupi, yanaonekana kuwa vigumu kuweza kuyafikia kirahisi. Hii ni kwa kuwa muundo wa kisiasa na kiuchumi wa Pakistan kwa miaka mingi umejengeka juu ya mfumo wa vyama viwili ambapo matakwa ya askari nayo yalizingatiwa, na kwa ajili hiyo kufikiwa mabadiliko anayoyataka kiongozi huyo mpya halitakuwa jambo rahisi. Kuhusiana na suala hilo, Nasser Ali Rahmani mtaalamu wa masuala ya kisiasa anasema: "Imran Khan, Waziri Mkuu mpya wa Pakistan atakuwa na taathira chanya kwenye mabadiliko ya ndani na nje ya Pakistan. Iwapo Khan ataweza kwenda sambamba na siasa za jeshi lake, basi atafanikiwa kufikia mipango yake." Hakuna shaka kwamba, Waziri Mkuu mpya wa Pakistan anakabiliwa na changamoto kadhaa kabla ya kuweza kutekeleza nara alizozitoa kwenye kampeni za uchaguzi kama vile kuboresha maisha ya wananchi, kuimarisha usalama na kutatua matatizo ya kieneo kwa ajili ya nchi hiyo. Kutumia nafasi za ndani na kadhalila za kieneo, kunaweza kumsaidia Imran Khan kuyafikia malengo hayo. Hakuna shaka kwamba kutekeleza mipango ya kiuchumi na kijamii, kunahitajia kuimarishwa kwanza usalama wa nchi kwa ajili ya kuvutia uwekezaji wa ndani na nje, mambo ambayo anayahitaji sana Waziri mkuu huyo mpya wa Pakistan.
Imran Khan kama mwanasiasa ambaye ameibuka kutoka katika makabila ya watu wa kati, anaweza kutumia nafasi za kieneo si tu katika kuimarisha usalama, bali hata katika kutatua matatizo ya kiuchumi likiwemo suala la nishati. Kwa vyo vyote vile, kwa mtazamo wa weledi wa masuala ya kisiasa, kuchaguliwa Khan kuwa Waziri Mkuu mpya wa Pakistan, ni fursa bora kwa ajili ya wanasiasa na shakhsia wa kisiasa ambao katika miaka iliyopita, waliwekwa kando ya ulingo wa kisiasa na ambapo sasa wanaweza kuendeleza harakati zao katika nyuga tofauti kwa ajili ya kupiga hatua za utatuzi wa matatizo ya nchi hiyo. Katika uwanja huo hakuna shaka kwamba hatua ya nchi jirani na Pakistan kutangaza utayarifu wao kwa ajili ya kushirikiana na Imran Khan hususan katika sekta ya nishati, kutamfungulia dirisha jipya kwa ajili ya kutatua matatizo ya nchi hiyo.