Russia yaionya tena Marekani juu ya kufanya shambulizi dhidi ya Syria
(last modified Thu, 30 Aug 2018 16:13:39 GMT )
Aug 30, 2018 16:13 UTC
  • Russia yaionya tena Marekani juu ya kufanya shambulizi dhidi ya Syria

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia ameelezea uwezekano wa Marekani na washirika wake kufanya shambulizi dhidi ya Syria hasa kwa kuzingatia hatua ya kusogezwa zana za kijeshi za nch hiyo katika eneo la Mashariki ya Kati.

Maria Zakharova ameyasema hayo Alkhamisi ya leo ambapo ameashiria njama za muungano vamizi wa Magharibi unaoongozwa na Marekani kwa ajili ya kufanya mashambulizi mapya  dhidi ya Syria na kuonya kuhusu hatma mbaya ya hujuma hiyo. Amesema kuwa, hatua ya kusogezwa zana za kijeshi katika eneo hilo ina maana kwamba, Washington na washirika wake wanaweza kufanya shambulizi dhidi ya Syria ndani ya kipindi cha masaa 24 yajayo.

Baadhi ya mashambulizi ya nchi za Magharibi yaliyofanywa dhidi ya Syria huko nyuma

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia sambamba na kueleza wasiwasi wake kuhusu uwezekano wa kukaririwa mchezo mchafu na wa kichochezi kwa kutumia madai bandia ya silaha za kemikali kama wenzo wa kuishambulia Syria, amesema kuwa, shambulizi kama hilo litakuwa pigo zito kwa juhudi za utatuzi wa mgogoro wa nchi hiyo na hata amani ya duniani. Maria Zakharova amesisitiza kuwa ni vigumu kutabiri hatma ya kuchezea moto.

Siku chache zilizopita pia, Wizara ya Ulinzi ya Russia ilionya kwamba Marekani imeimarisha zana zake za kijeshi karibu na Syria na kwamba hatua hiyo inakusudia kufanya shambulizi dhidi ya jeshi la serikali ya Damascus kwa kisingizio cha shambulizi bandia la silaha za kemikali.