Donald Trump amevunja rekodi ya kusema uongo
https://parstoday.ir/sw/news/world-i48122-donald_trump_amevunja_rekodi_ya_kusema_uongo
Gazeti maarufu la Washington Post la nchini Marekani limesema kuwa, rais wa nchi hiyo Donald Trump amevunja rekodi zote za kusema uongo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 13, 2018 23:01 UTC
  • Donald Trump amevunja rekodi ya kusema uongo

Gazeti maarufu la Washington Post la nchini Marekani limesema kuwa, rais wa nchi hiyo Donald Trump amevunja rekodi zote za kusema uongo.

Gazeti hilo limeanzisha kampeni maalumu ya kufuatilia uongo unaoenezwa na Trump kupitia matamshi na hotuba zake na kuandika kuwa, hadi hivi sasa Donald Trump ameshatoa zaidi ya matamshi elfu tano yasiyo na ukweli.

Gazeti hilo maarufu la Marekani limesema, Trump amekuwa akisema uongo kupindukia hasa katika takwimu anazozitoa na hivi sasa amejitengenezea rekodi mpya ya kusema uongo na kupiku rekodi zote za huko nyuma.

Rais wa Marekani, Donald Trump analaaniwa katika kila kona ya dunia

 

Kwa mujibu wa gazeti la Washington Post, kati ya dakika 120 za hotuba iliyotolewa na Trump Ijumaa iliyopita ya tarehe 7 Septemba, rais huyo wa Marekani alisema uongo mara 125 na hiyo ni rekodi mpya ya kusema uongo kwa siku moja. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Donald Trump huwa anasema uongo kwa wastani wa mara 7.3 kwa siku.

Washington Post limeongeza kuwa, tarehe 6 Septemba pia, Trump alisema uongo na mambo ya upotoshaji katika masuala 74 kwenye hotuba yake na sehemu kubwa ya uongo huo aliueneza mbele ya wafuasi wake huko Montana, magharibi mwa Marekani.

Hadi hivi sasa Donald Trump ameshasema uongo mara 5,001 katika kipindi cha siku 601 tangu awe rais wa Marekani ukijumuisha rekodi ya kusema uongo aliyoivunja katika siku mbili za tarehe 6 na 7 Septemba 2018.

Gazeti la Washington Post aidha limeripoti kuwa, kadiri siku zinavyopita ndivyo Trump anavyozidi kusema uongo tangu alipoingia madarakani huko Marekani.