Trump azishauri nchi za Ulaya kujenga ukuta katika Jangwa la Sahara.
Katika kuendeleza siasa zake zilizo dhidi ya uhamiaji na huku akiamini kwamba ujenzi wa kuta ndiyo njia bora zaidi ya kukabiliana na suala hilo, Rais Donald Trump wa Marekani amezishauri nchi za Ulaya kujenga ukuta katika Jangwa la Sahara ili kukabiliana na wimbi la wahajiri wa Kiafrika wanaohama nchi zao kuelekea nchi hizo.
Kwa mujibu wa video ambayo imekuwa ikisambazwa na vyombo vya habari vya Uhispania, Trump alitoa pendekezo la kujengwa ukuta huo baina ya mabara mawili ya Afrika na Ulaya kwa ajili ya kuwazuia wahajiri haramu wa Kiafrika kuelekea Ulaya, alipokuwa akizungumza na Joseph Borrel Waziri wa Mambo ya Nje wa Uhispania. Pendekezo hilo limetolewa na Trump katika hali ambayo tokea aingie madarakani na hata katika nara zake za kampeni za uchaguzi wa rais, amekuwa akisisitiza ujenzi wa ukuta baina ya nchi yake na Mexico ili kuzuia kuingia nchini humo wahamiaji haramu. Trump anaamini kwamba ili kuzuia kuingia Marekani wajahiri wanaotumia mpaka wa nchi hiyo na Mexico, ukuta unapaswa kujengwa katika mpaka wake wa kusini ulio na urefu wa kilomita 3200, suala ambalo limezua mvutano mkubwa baina ya nchi mbili hizo jirani.
Pendekezo la kujengwa kuta baina ya nchi tofauti linatolewa na Trump katika hali ambayo katika miaka ya hivi karibuni nchi nyingi za dunia zimekuwa zikiamini kwamba siasa za pande kadhaa na za kuimarisha ushirikiano wa kieneo na kimataifa zinaweza kutatua migogoro na changamoto nyingi na wakati huohuo kuimarisha maisha ya jamii nyingi uliwenguni. Kuhusiana na suala hilo, kuimarishwa amani, usalama, uchumi na kupunguza pengo la tofauti za kijamii pamoja na kuboresha hali ya maisha na afya katika ngazi za kimataifa ni jambo linaloweza kuwa na taathira kubwa katika kupunguza wimbi la uhamiaji haramu duniani. Ni kutokana na ukweli huo ndio maana nchi nyingi zimekuwa zikitekeleza siasa za kuchangia maenedeleo na kuimarisha maisha katika maeneo yenye migogoro yakiwemo ya Afrika, kupitia mashirika ya kimataifa.
Katika miaka ya hivi karibuni, kuongezeka vitendo vinavyovuruga usalama na kutokea mapigani katika baadhi ya maeneo ya Afrika, kuongezeka makundi ya kigaidi, mabadiliko ya tabianchi, kiangazi, kuzuka magonjwa hatari ya kuambikiza, uhaba wa chakula na vifaa vya afya na tiba na vilevile mabadiliko ya kisasa katika baadhi ya nchi za kieneo ni mambo ambayo yamechangia ongezeko la uhamiaji haramu kutoka nchi za Kiafrika kuelekea Ulaya. Hata kama hilo ni tatizo kubwa kwa nchi za Ulaya lakini ujenzi wa ukuta baina ya nchi hizo na za Afrika hauonekani kuwa utatuzi wa msingi wa tatizo hilo linaloongezeka kila uchao. Angela Merkel, Kensela wa Ujerumani anasema kuhusu jambo hilo kwamba hatuhitaji kuwa na ulimwengu ambao una kuta bali ulimwengu ambao kuta zinabomolewa ili kuwezesha watu wote kuishi maisha bora na ya heshima.
Hakika pendekezo la 'kujenga kuta kwenye mipaka' linapaswa kutathminiwa katika mtazamo mpana wa siasa za upande mmoja za Trump na nara yake ya 'Marekani Kwanza'.
Antonio Gutarres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anasema kuhusiana na jambo hilo kwamba changamoto zinazotukabili kwa sasa ni za kimataifa na iwapo hatutatumia mbinu za kimataifa kukabiliana nazo ni wazi kuwa hatutafanikiwa kuzitatua.
Ni wazi kuwa pendekezo la Trump la kujengwa ukuta baina ya nchi za Kiafrika na Ulaya limetolewa kutokana na siasa zake za upande mmoja na za kujiona kuwa mbora kuliko watu wengine. Hii ni katika hali ambayo mfumo wa sasa wa dunia haukubali tena siasa hizo za upande mmoja, ubabe na ujenzi wa kuta baina ya mataifa.