Wamarekani: Korea Kaskazini haijasimamisha miradi yake ya nyuklia!
(last modified Sun, 07 Oct 2018 02:26:57 GMT )
Oct 07, 2018 02:26 UTC
  • Wamarekani: Korea Kaskazini haijasimamisha miradi yake ya nyuklia!

Watafiti kadhaa ya Marekani wamedai kwamba, uchunguzi wao umebaini kuwa Korea Kaskazini inaendelea na shughuli zake za nyuklia huku ikiilaumu Washington kuwa inapuuza kutekeleza makubaliano yaliyofikiwa katika mkutano wa viongozi wa nchi hizo mbili mwezi Juni mwaka huu.

Watafiti hao wa Marekani wanadai kuwa, picha za satalaiti zinaonesha kuwa Kituo cha Utafiti wa Kisayansi wa Nyuklia cha Yongbyon huko Korea Kaskazini kinaendelea kufanya kazi.

Kundi hilo la watafiti wa Marekani limedai kuwa, picha zilizopigwa Septemba 24 mwaka huu zinaonesha kuweko harakati za kiwango cha chini za magari na vifaa katika eneo hilo ingawa wameshindwa kujua harakati hizo zilikuwa ni za kazi gani. Pamoja na hayo watafiti hao wamesema, kinu cha nyuklia ya Yongbyon hakikuwa kikifanya kazi wakati zilipopigwa picha hizo kwani hakuna moshi wowote uliokuwa unatoka kwenye kinu hicho.

Moja ya picha za satalaiti zilizotolewa na watafiki wa Marekani Oktoba 5, 2018 wakidai kuwa Kituo cha Utafiti wa Kisayansi wa Nyuklia cha Yongbyon cha Korea Kaskazini kinaendelea kufanya kazi.

 

Viongozi wa Marekani na Korea Kaskazini walionana kwa mara ya kwanza nchini Singapore mwezi Juni mwaka huu na kufikia makubaliano maalumu ambayo hata hivyo utekelezaji wake unakwenda kwa kasi ndogo.

Korea Kaskazini imesema imekubali kusimamisha shughuli za kituo cha nyuklia cha Yongbyon lakini kwa sharti kwamba Marekani nayo ichukue hatua za wazi za kutekeleza vipengee vya makubaliano yaliyofikiwa baina ya pande mbili.

Vile vile imekuwa ikisisitiza mara kwa mara kuwa Marekani haina mwamana kwani imesaliti moyo wa mkutano wa mwezi Juni wa viongozi wa nchi hizo mbili, kwa kukataa kuiondolea vikwazo Korea Kaskazini.

Pia Pyongyang inasisitiza kuwa, suala la kuachana na miradi yake ya nyuklia linapaswa kwenda hatua kwa hatua tena liende sambamba na Marekani kutekeleza makubaliano ya pande mbili hasa hasa kuondoka wanajeshi wa Marekani huko Korea Kusini na kuondolewa vikwazo kimoja baada ya kingine.

Tags