Nikki Haley, balozi wa Marekani UN ajiuzulu, Trump aridhia
https://parstoday.ir/sw/news/world-i48684-nikki_haley_balozi_wa_marekani_un_ajiuzulu_trump_aridhia
Rais Donald Trump wa Marekani amekubali uamuzi wa kujiuzulu balozi wa nchi hiyo katika Umoja wa Mataifa, Nikki Haley.
(last modified 2026-03-03T12:46:59+00:00 )
Oct 09, 2018 13:01 UTC
  • Nikki Haley, balozi wa Marekani UN ajiuzulu, Trump aridhia

Rais Donald Trump wa Marekani amekubali uamuzi wa kujiuzulu balozi wa nchi hiyo katika Umoja wa Mataifa, Nikki Haley.

Maafisa katika Ikulu ya White House wametangaza leo kuwa, Trump amekubali uamuzi wa mwakilishi wa nchi hiyo katika Umoja wa Mataifa Nikki Haley kujiuzulu wadhifa wake huo.

Kwa mujibu wa maafisa hao, Bi Haley alimtaarifu rais wa Marekani kuhusu uamuzi wake huo alipokutana naye wiki iliyopita Ikulu ya White House.

Nikki Haley

Baada ya Trump kuapishwa kuwa rais wa Marekani mapema mwaka uliopita wa 2018, Nikki Haley aliidhinishwa na Seneti ya nchi hiyo kushika wadhifa wa balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa.

Sababu iliyomfanya Bi Haley achukue uamuzi wa kujiuzulu wadhifa wake huo hadi sasa bado haijatangazwa, lakini inasemekana kuwa uamuzi huo umewashtusha maafisa waandamizi wa serikali ya Trump.

Kwa mujibu wa baadhi ya ripoti, yumkini sababu ya kujiuzulu Nikki Haley inahusiana na mauaji ya Jamal Khashoggi, mwandishi wa habari raia wa Saudi Arabia aliyekuwa mpinzani na mkosoaji wa utawala wa Aal Saud.

Aidha baadhi ya vyombo vya habari vya Marekani vimeripoti kuwa kung'atuka balozi wa nchi hiyo katika Umoja wa Mataifa kumetokana na tuhuma za kupokea rushwa.

Inafaa kuashiria kuwa idadi ya maafisa wa serikali ya Marekani waliojiuzulu wenyewe au kuuzuliwa katika kipindi cha urais wa Donald Trump ni kubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa katika historia ya nchi hiyo.../