Mkaguzi wa serikali ya Marekani ataka kuchunguzwa sababu za kujiuzulu Halley
Mkaguzi wa serikali ya Marekani ametoa wito wa kufanyika uchunguzi kuhusu sababu za kujiuzulu mwakilishi wa nchi hiyo katika Umoja wa Mataifa.
Ripoti iliyotolewa na mkaguzi wa serikali ya Marekani imetaka kufanyike uchunguzi kuhusu hatua ya Nikki Haley ya kujiuzulu ghafla na kuacha nafasi yake kama balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa.
Ripoti zinasema kuwa, kuna uwezekano kwamba, sababu za kujiuzulu Halley zinahusiana na mauaji ya mwandishi habari na mkosoaji mkubwa wa utawala wa kifalme wa Saudi Arabia, Jamal Khashoggi. Baadhi ya vyombo vya habari vya Marekani pia vinasema kuwa, Nikki Haley amejiuzulu kutokana na kashfa ya kula rushwa.
Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa alitangaza ghafla habari ya kujiuzulu kwake jana na kusema yumkini kwamba hafurahishwi na hatua za serikali ya nchi hiyo lakini anaziheshimu.
Rais Donald Trump amekubali uamuzi wa mwakilishi wa nchi hiyo katika Umoja wa Mataifa ya kujiuzulu wadhifa wake.
Haley ambaye alikuwa mkosoaki mkubwa wa Donald Trump katika kampeni za uchaguzi wa rais wa Marekani mwaka 2016, aliteuliwa na kiongozi huyo kuwa mwakilishi wa nchi hiyo katika Umoja wa Mataifa baada ya Trump kushinda kinyang'anyiro hicho.
Haley ni miongoni mwa maafisa wenye uhasama na misimamo mikali dhidi ya Iran wa Marekani na ndiye aliyekuwa mhamasishaji mkubwa wa fikra kuhamishiwa ubalozi wa Marekani katika mji wa Quds kutoka Tel Aviv, huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu.