Oct 13, 2018 11:55 UTC
  • Vikwazo vya kongresi ya Marekani dhidi ya Hizbullah ya Lebanon

Katika kuendelea jitihada za Marekani za kukabiliana na harakati ya mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon; kongresi ya nchi hiyo imepasisha mswada wa kuiwekea vikwazo vipya harakati hiyo.

Mike Crapo Mkuu wa Kamati ya Masuala ya Benki katika Seneti ya Marekani ametangaza kuwa kongresi ya nchi hiyo imepasisha mswada kwa lengo la kuiwekea Hizbullah ya Lebanon na baadhi ya nchi  vikwazo vipya. Ameongeza kuwa vikwazo hivyo vitazilenga pia nchi za nje, taasisi za kiserikali, mashirika au shakhsia ajinabi ambao wanaiunga mkono Hizbullah.  

Mike Crapo, Mike Crapo Mkuu wa Kamati ya Masuala ya Benki katika Seneti ya Marekani

Mswada huo ambao umeungwa mkono na vyama vyote viwili vya Republican na Democrat kwanza unapasa kusainiwa na Rais Donald Trump ili kuwa sheria. Marekani na waitifaki wake kwa muda mrefu sasa wamekuwa wakitumia mbinu mbalimbali kupambana na harakati ya Hizbullah ya Lebanon kwa sababu harakati hiyo siku zote imekuwa ikikabiliana kikamilifu na  Wazayuni maghasibu. Harakati ya Hizbullah ya Lebanon si tu kuwa imekuwa pamoja na bega kwa bega na wananchi madhlumu wa Palestina katika mapambano yao dhidi ya utawala unaokalia Quds kwa mabavu na ambao unaungwa mkono kwa pande zote na washington na utawala wa Saudi Arabia, bali hivi sasa  harakati hiyo ina nafasi muhimu pia katika kuendesha muqawama dhidi ya makundi ya kigaidi yanayoungwa mkono na Marekani, Saudia na waitifaki wao katika eneo hili.  

Kwa msingi huo, nafasi ya kisiasa na kijeshi iliyonayo harakati hiyo ya muqawama dhidi ya mirengo ya kigaidi na kitakfiri huko Iraq na Syria imeipelekea serikali ya Marekani kufanya juhudi maradufu ili kuizidishia mashinikizo Hizbullah kupitia vikwazo. 

Tamir Pardo mmoja wa wakuu wa zamani wa Shirika la Ujasusi la Israel  (Mossad) anasema kuhusu suala hilo kuwa: Ushindi wa kijeshi wa Israel mbele ya harakati ya Hizbullah ya Lebanon uko mbali na inavyodhaniwa na njia pekee ya kujiondoa kwenye mkwamo ni kuiwekea Lebanon vikwazo.   

Viongozi wa Washington wanadai kuwa hatua zinazotekelezwa na Hizbullah  zinasababisha ukosefu wa uthabiti wa kisiasa na kiuchumi katika eneo hili na kwamba ni tishio lisilo la kawaida kwa siasa za nje na usalama wa taifa wa Marekani. Ni wazi kuwa serikali ya Marekani inafanya kila iwezalo ili kuliweka chini ya udhibiti wake kikamilifu eneo hili nyeti na la kistratejia baada ya kusambaratika Daesh. Marekani aidha inataka kukabidhi uendeshaji wa masuala ya Mashariki ya Kati kwa waitifaki wake zikiwemo utawala wa Saudia na Israel hata hivyo ni muhali kufikiwa lengo hili kwa kuzingatia kuendelea kusimama kidete na kujizatiti mrengo wa muqawama unaozijumuisha Iran, Syria, Iraq na harakati ya Hizbullah ya Lebanon. Kwa msingi huo katika miezi ya karibuni si tu kuwa mashinikizo yameongezeka kwa Hizbullah bali viongozi wa Marekani wanafanya kila wanachoweza ili kutimiza malengo yao katika Mashariki ya Kati ikiwa ni pamoja na kuiwekea Iran vikwazo vizito na sasa, Hizbullah. 

Sayyid Hassan Nasrullah Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon anasema kuhusiana na kadhia hii kwamba: Vikwazo hivi haviathiri hali ya kifedha ya shakhsia ambao wameorodheshwa katika faharasa ya vikwazo; kwa sababu sisi hatuna fedha kwenye benki. Moja ya malengo ni kuwaweka mbali wananchi na sisi. Kwa hakika suala hili ni vita vya kisaikolojia  ambavyo vinawaathiri wananchi wa Lebanon. 

Sayyida Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon

Ni wazi kuwa Marekani na waitifaki wake katika eneo hili ukiwemo utawala wa Israel na Saudi Arabia zina wasiwasi kuhusu nafasi ya Hizbullah katika kupambana na ugaidi katika eneo la Asia Magharibi. Hii ni kwa sababu nafasi hiyo ya Hizbullah kwa upande mmoja imezizuia pande hizo kuendeleza uwepo wao katika eneo; na katika upande mwingine imepelekea kupata nguvu mhimili wa muqawama katika eneo. Kwa msingi huo kukabiliana na harakati ya Hizbullah ya Lebanon ni hatua ya awali inayotekelezwa na Marekani ili kuasisi mfumo unaoutaka katika eneo la Asia Magharibi na kupasisha vikwazo  pia kunaweza kutajwa kuwa ni sehemu ya siasa hizo za Washington.  

Tags