Oct 24, 2018 02:51 UTC
  • Australia yawewekea vikwazo makamanda wa jeshi la Myanmar

Serikali ya Australia imetangaza kuwawekea vikwazo makamanda watano wa jeshi la Myanmar wanaotuhumiwa kuongoza mauaji na jinai dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Australia, Marise Payne amesema watano hao Aung Kyaw Zaw, Maung Maung Soe, Aung Aung, Than Oo na Khin Maung Soe ndio wanaopaswa kubebeshwa dhima ya jinai hizo za kutisha dhidi ya Warohigya, kwani ndio waliowaagiza askari chini vikosi vyao kuwashambulia Waislamu Warohingya.

Mbali na mali zao kufungiwa, makamanda hao wa ngazi za juu wa jeshi la Myanmar pia hawataruhusiwa kutia mguu nchini Australia.

Mara kadhaa shirika la kutetea haki za binadmau la Human Rights Watch (HRW) limeripoti kuwa,  jeshi la Myanmar linawaua kiholela na kuwanajisi Waislamu wa jamii ya Rohingya katika mkoa wa Rakhine, magharibi mwa nchi hiyo.

Hii ni katika hali ambayo, mashirika ya kimataifa yasiyo ya serikali yanasema kuwa hatua za serikali ya Myanmar dhidi ya Waislamu wa Rohingya ni jinai za wazi dhidi ya binaadamu ambapo sambamba na kulaani jinai hizo yameitaka dunia kukabiliana na serikali ya nchi hiyo ili kuzuia hali hiyo.

Wanajeshi katili wa Myanmar

Maelfu ya Waislamu wa kabila la Rohingya nchini Myanmar wameuawa na maelfu ya wengine kujeruhiwa tangu kuanza wimbi jipya la mashambulizi ya jeshi na Mabudha wenye misimamo mikali katika mkoa wa Rakhine magharibi mwa nchi hiyo tangu tarehe 25 Agosti mwaka jana hadi sasa. 

Mauaji hayo ya umati dhidi ya Waislamu nchini Myanmar yamepelekea zaidi ya laki nane miongoni mwao kukimbilia hifadhi katika nchi jirani za Bangladesh na India.

Tags