Susan Rice awataka waandishi wa habari kususia vikao vya White House
https://parstoday.ir/sw/news/world-i49402-susan_rice_awataka_waandishi_wa_habari_kususia_vikao_vya_white_house
Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Rais wa zamani wa Marekani, Susan Rice amewataka waandishi wa habari kususia vikao vya habari vya ikulu ya Rais wa Marekani, White House hadi pale ikulu hiyo itakapojirekebisha kuwahusu.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Nov 09, 2018 23:07 UTC
  • Susan Rice
    Susan Rice

Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Rais wa zamani wa Marekani, Susan Rice amewataka waandishi wa habari kususia vikao vya habari vya ikulu ya Rais wa Marekani, White House hadi pale ikulu hiyo itakapojirekebisha kuwahusu.

Susan Rice aliyekuwa Mshauri wa Usalama wa Taifa kipindi cha Barack Obama, ametoa wito huo kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter katika radiamali yake kufuatia hatua ya White House ya kabatilisha kibali cha kuingia ikulu hiyo mwandishi wa habari wa televisheni na CNN, ambapo amewataka waandishi wa habari kususia vikao vya ikulu. Katika ujumbe huo Rice ameandika kuwa: "Umefika wakati kwa jumuiya ya waandishi wa habari kususia vikao vya habari vya White House na madamu bado haijakomesha mienendo yake dhidi ya waandishi wa habari, basi hatutorudi tena ikulu hiyo."  Amesema. 

Mwito huo wa Susan Rice umetolewa wakati ambao serikali ya Marekani imefuta kibali cha kuingia ikulu ya White House cha Jim Acosta, mwandishi wa habari wa Shirika la Habari la CNN kwa tuhuma ya kumkosea adabu Rais Donald Trump.

Mwandishi wa habari wa CNN alipomuhoji Trump na kubatilishwa kibali chake

Jumatano iliyopita, na katika kikao cha waandishi wa habari ndani ya White House, Acosta alimuhoji rais huyo kuhusiana na siasa zake dhidi ya wahajiri. Kufuatia swali hilo Trump katika hatua isiyo ya kawaida na kinyume na maadili ya kibinaadamu na kisiasa, alimvunjia heshima mwandishi huyo wa habari wa CNN ambapo sambamba na kukatisha swali lake, alimtaka msimamizi wa kikao kumnyang'anya mikrofoni Jim Acosta. Inafaa kuashiria kuwa, kwa muda sasa Trump amekuwa na misimamo hasi dhidi ya kanali ya televisheni ya CNN na mashirika mengine ya habari ya nchi hiyo kwa madai kwamba vyombo hivyo vinaeneza uongo.