Trump ailaumu Democrats kwa vifo vya watoto wahajiri waliokuwa kizuizini
https://parstoday.ir/sw/news/world-i50526-trump_ailaumu_democrats_kwa_vifo_vya_watoto_wahajiri_waliokuwa_kizuizini
Rais Donald Trump wa Marekani amekilaumu chama cha upinzani cha Democrats kwa vifo vya watoto wawili wahajiri walipoteza maisha hivi karibuni wakiwa kizuizini ndani ya ardhi ya nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 30, 2018 23:11 UTC
  • Trump ailaumu Democrats kwa vifo vya watoto wahajiri waliokuwa kizuizini

Rais Donald Trump wa Marekani amekilaumu chama cha upinzani cha Democrats kwa vifo vya watoto wawili wahajiri walipoteza maisha hivi karibuni wakiwa kizuizini ndani ya ardhi ya nchi hiyo.

Akizungumzia vifo hivyo kwa mara ya kwanza hapo jana, Trump amesema watoto hao walikuwa wagonjwa sana kabla ya kuingia nchini humo. Trump amelaumu kile alichokitaja kama sera mbaya za Wademocrats wanaoruhusu watu kutembea mafasa marefu na kuingia nchini humo kinyume cha sheria, pasina na kufanyiwa ukaguzi.

Hii ni licha ya Idara ya Forodha na Hifadhi ya Mipaka ya Marekani kuwafanyia uchunguzi wa kitiba wahajiri wote wanaoingia nchini humo kupitia mipakani wakiwemo watoto wao.

Siku chache baada ya kufariki dunia Jakelin Caal Maquin, binti aliyekuwa na umri wa miaka saba mhajiri kutoka Guatemala aliyekuwa akishikiliwa kizuizini nchini Marekani, Idara ya Wakala wa Forodha na Hifadhi ya Mipaka ya nchi hiyo mkesha wa Krismasi ilitangaza habari ya kufariki dunia mtoto mwingine mhajiri aliyekuwa na umri wa miaka 8 katika kizuizi cha wakala huo. 

Watoto wa wahajiri waliotengwa na wazazi wao nchini Marekani

Catarina Alonzo, mama ya mtoto wa miaka 8 raia Guetemala aliyefariki dunia, kwa jina Felipe Gomez Alonzo amesema mwanawe hakuwa na ugonjwa wowote, na alifika katika mpaka wa nchi hiyo na Marekani akiwa salama salmin.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu likiwemo shirika la Amnesty International yamekosoa sera za kikatili za serikali ya Marekani kuhusiana na wahajiri na kutoa wito wa kubadilishwa mwenendo huo.