UNICEF: Watoto Milioni 41 duniani wanahitaji msaada wa dola bilioni 3.9
(last modified Wed, 30 Jan 2019 01:09:46 GMT )
Jan 30, 2019 01:09 UTC
  • UNICEF: Watoto Milioni 41 duniani wanahitaji msaada wa dola bilioni 3.9

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF limesema linahitaji msaada wa dola bilioni 3.9 ili kuwasaidia watoto milioni 41 walio katika maeneo ya majanga kote duniani.

Katika taarifa ya Jumanne huko Geneva, Uswisi, UNICEF imesema mamilioni ya watoto wanaoishi katika nchi zilizoathiriwa na migogoro na majanga wanakosa huduma muhimu za ulinzi na hivyo usalama na mustakabali wao uko hatarini.

UNICEF imesema fedha hizo zinahitajika mwaka 2019 ili kusambaza maji safi na salama, lishe, elimu, huduma ya afya na ulinzi katika nchi 59 kote ulimwenguni.

Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Henrietta Fore amesema, leo mamilioni ya watoto wanaoishi katika mizozo na majanga wanakabiliwa na ukatili wa kusikitisha, dhiki na kiwewe.

Picha za watoto wa Yemen ambao wanauawa na wengine kukumbwa na matatizo makubwa kutokana na hujuma ya Saudia na waitifaki wake dhidi ya nchi hiyo

UNICEF inakadiria kuwa takriban watoto milioni 34 wanaoishi kwenye mizozo na majanga wanakosa huduma za ulinzi kukiwemo kuwaepusha na ukatili na kutelekezwa na huduma muhimu. Taarifa hiyo imebaini kuwa miongoni mwa watoto wanaohitajia misaada, watoto milioni 6.6 wako nchini Yemen, milioni 5.5 nchini Syria na milioni 4 wakiwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC.

UNICEF imetoa wito kwa jamii ya kimataifa kusaidia katika ufadhili huku likionya kuwa ukata huenda ukasababisha baadhi ya watoto kuachwa nyuma katika nyanja mbali mbali.