Uturuki yaitaka China ifunge vituo vya kuwazuilia Waislamu wa Uighur
https://parstoday.ir/sw/news/world-i51462-uturuki_yaitaka_china_ifunge_vituo_vya_kuwazuilia_waislamu_wa_uighur
Serikali ya Uturuki imetaja miamala ya China kwa Waislamu wa jamii ya Uighur kama fedheha kwa ubinadamu, huku ikiitaka ifunge vituo vilivyotengwa makhsusi kwa ajili ya kuwazuilia watu wa jamii hiyo ya walio wachache.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 10, 2019 09:54 UTC
  • Uturuki yaitaka China ifunge vituo vya kuwazuilia Waislamu wa Uighur

Serikali ya Uturuki imetaja miamala ya China kwa Waislamu wa jamii ya Uighur kama fedheha kwa ubinadamu, huku ikiitaka ifunge vituo vilivyotengwa makhsusi kwa ajili ya kuwazuilia watu wa jamii hiyo ya walio wachache.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki, Hami Aksoy amesema inasikitisha kuona Waislamu zaidi ya milioni moja wa Uighur wanazuiliwa kinyume cha sheria katika kambi hizo zilizoko magharibi mwa China.

Amebainisha kuwa, "Sio siri tena Waislamu zaidi ya milioni moja wa jamii ya Uighur wenye asili ya Uturuki wanazuiliwa katika mazingira magumu, huku wakikandamizwa na utamaduni wao wa Kiislamu ukioanishwa na Ukomunisti."

Ameongeza kuwa, ni muhali kutekeleza sheria na ibada za Kiislamu nchini China hasa katika mkoa wa Xinjiang ambao una Waislamu zaidi ya milioni 10, huku akiitaka serikali ya Beijing iheshimu haki za msingi za binadamu na uhuru wa kuabudu.

Ukandamizaji dhidi ya Waislamu wa Uighur nchini China

Inafaa kuashiria kuwa, serikali ya Beijing na kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi, imeanzisha vituo kadhaa katika mkoa huo wa Xinjiang ambavyo vimekuwa vikitumika katika kuwazuilia ndani yake Waislamu wa jamii hiyo.

Hata hivyo China imetoa ripoti kadhaa za kupinga uchunguzi wa timu ya Umoja wa Mataifa uliothibitisha kwamba karibu Waislamu milioni moja wa jamii ya Uighur wanazuiliwa na maafisa usalama wa nchi hiyo.