Guterres: Wasichana wa vijijini wapewa fursa ya kusoma
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametoa mwito wa kufanywa jitihada na kuandaliwa mikakati maalumu kwa ajili ya kuwapa elimu watoto wa kike hususan wanaoishi vijijini.
Antonio Guterres amesema hayo katika ujumbe alioutoa kwa mnasaba wa Siku ya Kimataifa ya Wasichana na Wanawake katika Sayansi inayoadhimishwa kote duniani hii leo (Februari 11).
Amesema dunia haipaswi kupoteza fursa ya kupokea na kujumuisha mchango wa nusu ya idadi ya watu duniani, iwapo inataka kupiga hatua katika uga wa elimu.
Katibu Mkuu wa UN amefafanua kwa kusema, "Ujuzi katika masomo ya sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati ni katika ubunifu na chachu ya kufikiwa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG's)."
Antonio Guterres amebainisha kuwa, mfumo dume, taasubi za kijinsia, sera kandamizi na kunyimwa fursa au kukosekana mazingira mazuri ni katika mambo yanayoweza kuwafanya wanawake na watoto wa kike washindwe kujiimarisha kielimu.
Ameitaka dunia ipambane na vikwazo na vizingiti katika kufanikiwa kielimu mtoto wa kike hasa wa kijijini, na kumwezesha kufikia ndoto yake ya kuwa mwanasayansi, mhandisi au hata mwanahesabati, bila ya kumbeza na kumuona duni.