Tuhuma mpya za Marekani kwa Pakistan kuhusiana na uungaji mkono ugaidi
Kwa mara nyingine Kamanda Mkuu wa Kamandi ya Jeshi la Marekani ameituhumu serikali ya Pakistan kwamba inaunga mkono makundi ya kigaidi na kuyapa hifadhi.
Joseph Leonard Votel kwa mara nyingine amewataka viongozi wa Pakistan kuharibu maficho yote ya makundi ya kigaidi sambamba na kuwaangamiza magaidi hao wanaoendeshea harakati zao ndani ya ardhi ya nchi hiyo. Matamshi ya kamanda huyo wa jeshi la Marekani dhidi ya Islamabad yametolewa katika hali ambayo Ahsan Iqbal, Waziri wa Zamani wa Mambo ya Ndani wa Pakistan amenukuliwa akisema kuwa, Marekani haina uwezo wa kudhamini usalama na amani nchini Afghanistan na ni kwa ajili hiyo ndio maana inaituhumu serikali ya Islamabad kwamba inaunga mkono makundi ya kigaidi. Baada ya kuingia madarakani serikali ya Rais Donald Trump wa Marekani, Washington ilianzisha wimbi la tuhuma dhidi ya Pakistan kwamba inaunga mkono magenge ya kigaidi na kuchochea machafuko yanayoendelea nchini Afghanistan, tuhuma ambazo zimekuwa zikikanushwa vikali na Islamabad. Matamshi hayo ya Kamanda Mkuu wa Kamandi ya Jeshi la Marekani, Joseph Leonard Votel dhidi ya Pakistan yanaakisi siasa za kigeni za ikulu ya White House za kukabiliana na Islamabad katika miaka ya hivi karibuni. Inafaa kukumbusha kwamba uhusiano wa Washington na Islamabad ulianza kuingia doa tangu mwaka 2004 na baada ya hatua za upande mmoja za Marekani za kuendesha mashambulizi ya ndege zake zisizo na rubani katika maeneo ya makabila ya Pakistan kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi.
Katika kipindi hiki, masuala mengine zikiwemo tuhuma kwamba Pakistan inayaunga mkono makundi ya kigaidi au kuendesha vita vya niaba nchini Afghanistan na India, yamezidi kuharibu mzozo wa pande mbili hizo. Kwa mtazamo wa Marekani, sababu kuu ya kushindwa askari wa kigeni nchini Afghanistan katika kukabiliana na ugaidi, ni siasa za undumakuwili za Pakistan katika kuamiliana na makundi yenye misimamo mikali. Ni kwa kutumia madai hayo ndipo serikali ya sasa ya Marekani chini ya Rais Donald Trump, ikaamua kuzuia misaada ya kifedha na kijeshi ya White House kwa Islamabad. Katika uwanja huo, Sayyed Amin Behrad, mtaalamu wa masuala ya kisiasa wa Afghanistan anasema: "Uungaji mkono wa Pakistan kwa makundi ya kigaidi na uingiliaji wake wa masuala ya ndani ya Afghanistan, ni mambo ambayo yako wazi kwa kila mtu na dunia inatakiwa kuchukua hatua ya kivitendo dhidi ya Islamabad." Pamoja na kwamba tuhuma hizo sio jambo jipya kwa kuzingatia kuwa huko nyuma pia Marekani imekuwa ikiinyoshea kidole cha lawama serikali ya Pakistan kwamba inahusika na kuyaunga mkono makundi ya kigaidi, lakini kitendo cha kutolewa tuhuma hizo katika mazingira ya sasa wakati Pakistan na India hivi karibuni zilishuhudia mgogoro wa kijeshi, kinatathminiwa kuwa ni chenye ujumbe maalumu katika kuchochea mzozo huo. Mashambulizi ya hivi karibuni ya ndege za kijeshi za India katika maeneo ya Pakistan, ambayo yalijibiwa kwa ulipizaji kisasi wa Islamabad, yalitekelezwa kwa kisingizio cha kuharibu maficho ya kundi la kigaidi linalojiita Jaish-e-Mohammed, ambalo lilituhumiwa kuhusika na shambulizi la kigaidi eneo la Pulwama, jimbo la Kashmir linalodhibitiwa na India.
Aidha msimamo wa Kamanda Mkuu wa Kamandi ya Jeshi la Marekani, Joseph Votel katika kuituhumu tena Pakistan, na ambao umetolewa huku uhusiano wa Islamabad na New Delhi ukiwa umegubiwa na mgogoro, umetafsiriwa kuwa ni aina fulani ya Washington kutangaza uungaji mkono wake kwa India na pia kuhalalisha mashambulizi ya New Delhi dhidi ya Pakistan. Kwa hakika matamshi ya kiongozi huyo wa jeshi la Marekani ambayo yanaashiria uungaji mkono kwa India yanafikisha ujumbe huu kwamba, mashambulizi ya ndege zake za kijeshi katika ardhi za Pakistan, yalifanyika katika fremu ya kujilinda na kuharibu maficho ya kundi la kigaidi la eti Jaish-e-Mohammed. Inaonekana kwamba, matamshi ya Votel mbali na kwamba yanaweza kuishajiisha zaidi India kuunga mkono siasa za Washington katika eneo, yanaweza pia kuifanya Pakistan kuwa na nafasi katika kuharibu mipango ya Washington nchini Afghanistan.