Mamia waandamana London, Uingereza dhidi ya utawala haramu wa Israel
Mamia ya watu wamejitokeza katika barabara za London, mji mkuu wa Uingereza kushiriki maandamano dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel.
Maandamano hayo yalifanyika jana nje ya ubalozi wa utawala haramu wa Israel, kwa mnasaba wa kuadhimisha mwaka mmoja wa maandamano ya 'Haki ya Kurejea' na mwaka wa 43 wa 'Siku ya Ardhi ya Palestina' zilizoadhimishwa jana Jumamosi.
Katika maandamano ya London, waandamanaji walikuwa wamebeba mabango yaliyokuwa na jumbe za kuwaunga mkono wananchi madhulumu wa Palestina, na zingine za kuonyesha kutoridhishwa kwao na jinai wanazofanyiwa Wapalestina na utawala haramu wa Israel.
Aidha wananchi wa Jordan walifanya maandamano baada ya Swala ya Ijumaa iliyopita katika mji mkuu Amman, ili kuonesha uungaji mkono wao kwa wananchi wa Palestina ambao hapo jana walifanya maandamano makubwa ya kuadhimisha mwaka mmoja tangu yalipoanza maandamano hayo ya Haki ya Kurejea.
"Maandamano Makubwa ya Kurejea' yamekuwa yakifanyika kila wiki tokea Machi 30 mwaka jana na Wapalestina wamekuwa wakitaka utawala wa Kizayuni wa Israel usitishe ukaliaji wa mabavu wa ardhi zao. Aidha wanataka wakimbizi wote Wapalestina warejee katika ardhi zao za jadi.
Tangu maandamano hayo yaanze hadi sasa, zaidi ya Wapalestina 250 wameshauliwa shahidi na wengine wanaokaribia 30 elfu wamejeruhiwa.