Tishio la ufyatuaji risasi lapelekea kufungwa shule 19 nchini Marekani
(last modified Wed, 17 Apr 2019 07:30:45 GMT )
Apr 17, 2019 07:30 UTC
  • Tishio la ufyatuaji risasi lapelekea kufungwa shule 19 nchini Marekani

Kufuatia tishio la kufyatua risasi shuleni, polisi ya Marekani imetangaza hali ya hatari katika shule 19 za jimbo la Colorado

Polisi inamtafuta binti mmoja aliye na umri wa miaka 18 kwa jina la Sol Pais ambaye ametoa matamshi ya kutishia kufyatua risasi katika shule za jimbo hilo. Imesema kutokana na kutoeleweka vyema shule inayolengwa katika tishio hilo, polisi imeamua kufunga kwa muda shule ya sekondari ya Columbine na shule nyingine 18 katika jimbo hilo. Tarehe 20 Aprili 1999 wanafunzi wawili katika shule hiyo walifyatua risasi kiholela na kuwaua wanafunzi 12 na mwalimu mmoja. Polisi ya upelelezi ya FBI imesema kuwa Pais alifika jimboni hapo jana usiku na kwamba tayari alikuwa ameandaa silaha.

Usalama waimarishwa baada ya kutokea ufyatuaji risasi jimboni Colorado

Pais aliwasili katika mji wa Denver, ambao ni mji ulio na wakazi wengi zaidi jimboni hapo na kutoa matamshi ya vitisho, lakini hakusema ni shule gani angeishambulia. Kila mwaka maelfu ya watu katika pembe tofauti za Marekani hupoteza maisha au kujeruhiwa kutokana na ufyatuaji risasi. Ushawishi wa lobi zenye nguvu za utengenezaji silaha katika serikali na kongresi ya Marekani umevuruga juhudi zote zinazofanywa na makundi ya kutetea haki za binadamu zinazolenga kubuniwa sheria kali za kudhibiti umiliki wa silaha nchini humo.