Hatua mpya ya Marekani dhidi ya makubaliano ya JCPOA
(last modified Sat, 04 May 2019 11:08:19 GMT )
May 04, 2019 11:08 UTC
  • Hatua mpya ya Marekani dhidi ya makubaliano ya JCPOA

Makubaliano ya nyuklia ya JCPOA ni makubaliano muhimu sana katika fremu ya kulinda amani na usalama wa kimataifa; hata hivyo tarehe 8 mwezi Mei mwaka jana Marekani ilijitoa kwenye makubaliano hayo. Serikali ya Trump mwezi Agosti na Novemba mwaka 2018 katika marhala mbili iliiwekea tena Iran vikwazo vya nyuklia; na ingali inaendeleza mashinikizo ya vikwazo dhidi ya Tehran.

Marekani imefutilia mbali vibali vitatu vya shughuli za nyuklia za Iran katika hatua yake mpya dhidi ya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA; na wakati huo huo  kupunguza muda wa vibali vilivyosalia pia kutoka siku 180 hadi 90. Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Marekani jana usiku ilitangaza katika taarifa yake kuwa kuanzia leo Jumamosi tarehe Nne Mei ushirikiano wowote wa nchi ya tatu katika kuendeleza kiwanda cha nyuklia cha Bushehr au kusafirisha nje ya Iran urani iliyorutubishwa na maji mazito kutaifanya nchi hiyo ikabiliwe na vikwazo. Hata hivyo shughuli za taasisi za nyuklia za Bushehr, Arak na Fordo hazitaguswa na vikwazzo hivyo. Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Marekani aidha imesisitiza katika taarifa yake hiyo kuwa Washington haitaruhusu tena kuhifadhiwa maji mazito ya ziada ya Iran, mbali na maji mazito yaliyopo hivi sasa. Katika hali ambayo kwa mujibu wa makubaliano ya JCPOA; Iran inaruhusiwa kurutubisha urani katika kiwango cha asilimia 3.67, vikwazo vya karibuni vilivyowekwa na Marekani dhidi yake vina maana ya kutaka kusimamishwa shughuli za urutubishaji urani nchini Iran.  

Taasisi ya nyuklia ya Bushehr nchini Iran 
 

Taarifa hiyo inasema mwanzoni: Serikali ya Trump bado inaitambua Iran kuwa inatekeleza hatua ambazo ni tishio kwa eneo. Sera hiyo pia inakusudia kuizuia Iran kuchukua hatua yoyote inayoiwezesha kumiliki silaha za nyuklia.  

Kwa kutoa taarifa yake hiyo, Marekani kivitendo imezizuia nchi za kundi la 4+1 kutekeleza makubaliano hayo ya kimataifa kukiwemo kufanikishwa kusafirishwa nchini Oman maji mazito ya ziada kutoka Iran, kubadilishwa urani iliyorutubishwa na keki ya njano, na pia kukwamishwa ushirikiano wa  Russia katika kukiendeleza kituo cha nguvu za nyuklia cha Bushehr. 

Wakati huo huo Mike Pompeo Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani amedai kuwa maamuzi yao hayo yamechukuliwa ili kuizuia Iran kuchukua hatua yoyote kwa lengo la kumiliki silaha za nyukjlia. Pompeo ameyatamka hayo katika hali ambayo Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) hadi sasa umetoa ripoti 14 zinazothibitisha kuwa miradi ya nyuklia ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni ya malengo ya amani.  

Mike Pompeo, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani 

Ni wazi kuwa hatua mpya ya Marekani inakinzana kikamilifu na vipengee vya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa; bali zaidi hatua hiyo imechukuliwa kwa msingi wa matakwa ya kibabe ya serikali ya Washington ili kuzizuia nchi nyingine kushirikiana kwa vyovyote kinyuklia na Iran. Ni dhahir shahir kuwa serikali ya Trump sasa inajaribu kufanya kila iwezalo ili kusimamisha mojawapo ya masuala muhimu yaani kusitisha miradi ya nyuklia ya Iran kwa kutumia nguvu na mabavu kwa kuzingatia kuwa Iran ilipinga masharti 12 yaliyowasilishwa kwake na Pompeo mwaka jana. Marekani pia imepuuza ripoti zilizotolewa na Wakala wa IAEA kwamba miradi ya nyuklia ya Iran inafanyika kwa malengo ya amani; na badala yake kuzingatia madai ya uwongo ya utawala wa Kizayuni katika uwanja huo. Marekani imefanya hivyo ili kuiweka Iran  katika mashinikizo makubwa ya kisiasa. 

Pamoja na hayo, Iran imesimama kidete na kwa azma thabiti mbele ya mashinikizo ya Marekani na matakwa yake haramu. Nchi wanachama zinazounda kundi la 4+1 pia kinyume na inavyodai Marekani kuwa Iran haijatekeleza vipengee vya makubaliano ya JCPOA na kwamba haiyatambui makubaliano hayo kama yanayofaa na mazuri kwa ajili ya kudhibiti shughuli za nyuklia za Iran zinaamini kuwa, si tu kuwa Iran imetekeleza majukumu yake yote katika fremu ya makubaliano hayo ya nyuklia ya JCPOA bali makubaliano hayo yamefanikiwa pia kutimiza malengo yaliyokusudiwa, yaani kuzuia kuibuka mivutano na mizozo katika ngazi ya kieneo na kimataifa. Nchi wanachama wa kundi la 4+1 zinataka kutekelezwa vipengee vya makubaliano hayo ya nyuklia kukiwemo kuendeleza shughuli za nyuklia za Iran zenye malengo ya amani. 

Tags