Russia, Ujerumani na Ufaransa zasisitiza kuwa JCPOA lazima ilindwe
(last modified Wed, 22 May 2019 08:16:33 GMT )
May 22, 2019 08:16 UTC
  • Russia, Ujerumani na Ufaransa zasisitiza kuwa JCPOA lazima ilindwe

Viongozi wa Russia, Ujerumani na Ufaransa wamesisitizia haja ya kubakishwa hai na kulindwa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, huku wakibainisha kuwa nchi zao zinafanya kila linalowezekana kuimarisha uhusiano wao wa kibiashara na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, licha ya Marekani kuchukua hatua ya upande mmoja ya kujiondoa kwenye mapatano hayo ya kimataifa.

Ikulu ya Russia (Kremlin) imesema Rais wa nchi hiyo Vladimir Putin, Chansela wa Ujerumani Angela Merkel na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron waliyasema hayo katika mazungumzo yao ya simu ya jana Jumanne.

Viongozi hao wa Russia, Ujerumani na Ufaransa wamesisitiza kuwa wataendelea kuunga mkono makubaliano ya nyuklia ya Iran, ambapo wamebainisha kuwa mapatano hayo ni nukta muhimu katika uthabiti na usalama wa kimataifa.

Taarifa ya Kremlin imebainisha kuwa, nchi tatu hizo zimesema kuwa zitaendelea kufungamana na makubaliano ya JCPOA, na kushirikiana na Iran katika mabadilishano ya kibiashara, ikiwa ni sehemu ya vipengee muhimu vya mapatano hayo yaliyosainiwa mjini Vienna mwaka 2015.

Nchi zilizosalia ndani ya JCPOA baada ya Rais Donald Trump kuiondoa Marekani

Tarehe 31 Januari mwaka huu Umoja wa Ulaya na baada ya miezi kadhaa ya majadiliano na Tehran, hatimaye ulianzisha mfumo  maalumu wa kibiashara na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran uliopewa jina la  (INSTEX) ingawa tangu wakati huo EU imekuwa ikichelewesha utekelezwaji wa mfumo huo kwa visingizio mbalimbali.

Kutokana na hali hiyo, Rais Hassan Rouhani wa Iran mapema mwezi huu alisema kwamba Tehran imesitisha utekelezaji wa baadhi ya vipengee vya JCPOA, kukiwemo kuongeza akiba ya urani yake iliyorutubishwa pamoja na maji mazito ya nyuklia na kama katika kipindi cha siku 60 nchi za Ulaya zitashindwa kuchukua hatua za kukabiliana na vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran, basi Tehran itachukua hatua zaidi.

  

Tags