Bagladesh: Myamar haitaki kuwarejesha nchini wakimbizi wa Rohingya
Waziri Mkuu wa Bangladesh ameikosoa vikali serikali ya Myanmar kwa kutoonesha nia wala mpango wa kuwa tayari kuwapokea wakimbizi Waislamu wa Rohingya waliokimbilia nchini humo miaka miwili iliyopita.
Sheikh Hasina aliyasema hayo jana Jumatatu katika kikao na waandishi wa habari mjini Dhaka na kuongeza kuwa, "Tatizo liko upande wa Myanmar kwa kuwa hawataki kabisa kuwachukua wakimbizi."
Kadhalika amezikosoa taasisi za kimataifa ambazo zinawapa huduma mbalimbali wakimbizi hao wa Kirohingya wanaoshi kambini katika eneo la Cox’s Bazar, kusini-mashariki mwa Bangladesh kwa kukwamisha jitihada za kuwarejesha nyumbani wakimbizi hao.
Amesema taasisi hizo zinakwamisha juhudi za kuwarejesha nyumbani wakimbizi hao kutokana na wao kuweka mbele maslahi yao.
Hivi karibuni serikali ya Dhaka sambamba na kukosoa mwenendo wa serikali ya Myanmar wa kurefusha mambo na kutoa ahadi za uongo kuhusu kuwarejesha nyumbani wakimbizi Waislamu wa Rohingya, ilisema kuwa, kwa sasa Bangladesh haina uwezo tena wa kupokea mkimbizi yeyote.
Maelfu ya Waislamu wa kabila la Rohingya nchini Myanmar wameuawa na maelfu ya wengine kujeruhiwa tangu kuanza wimbi jipya la mashambulizi ya jeshi na Mabudha wenye misimamo mikali katika mkoa wa Rakhine magharibi mwa nchi nchi hiyo tangu tarehe 25 Agosti mwaka 2017 hadi sasa.
Mauaji hayo ya umati dhidi ya Waislamu nchini Myanmar yamepelekea karibu Waislamu milioni moja wa jamii ya Rohingya kukimbilia hifadhi katika nchi jirani ya Bangladesh.