Russia: Iran inapambana vilivyo na vitendo vya kigaidi
https://parstoday.ir/sw/news/world-i54259-russia_iran_inapambana_vilivyo_na_vitendo_vya_kigaidi
Katibu wa Baraza la Usalama wa Taifa la Russia ameunga mkono kuweko washauri wa kijeshi wa Iran nchini Syria na kusisitiza kuwa, washauri hao wa kijeshi wako nchini humo kwa mwaliko rasmi wa serikali ya Damascus.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 21, 2019 05:20 UTC
  • Russia: Iran inapambana vilivyo na vitendo vya kigaidi

Katibu wa Baraza la Usalama wa Taifa la Russia ameunga mkono kuweko washauri wa kijeshi wa Iran nchini Syria na kusisitiza kuwa, washauri hao wa kijeshi wako nchini humo kwa mwaliko rasmi wa serikali ya Damascus.

Nikolai Patrushev amenukuliwa na Klabu ya Waandishi wa Habari Vijana ya Iran akisema hayo na kusisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iko kisheria nchini Syria kwani imealikwa na serikali ya nchi hiyo kuisaidia Damascus kupambana na magenge ya kigaidi, hivyo ni wajibu wa kila mtu kuheshimu na kuzingatia maslahi ya Iran huko Syria.

Matamshi ya Katibu wa Baraza la Usalama wa Taifa la Russia yametolewa kwa mnasaba wa kikao cha maafisa wa ngazi za juu wa kiusalama wa Marekani, Russia na utawala wa Kizayuni, ambacho kinatarajiwa kufanyika wiki ijayo katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni.

Brigedia Jenerali Hossein Hamedani, mshauri wa kijeshi wa Iran aliyeuawa shahidi nchini Syria tarehe 7 Oktoba 2015

 

Kwa muda sasa kumekuwa na taarifa za vyombo vya habari vinavyotangaza kwamba Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel zinafanya njama kubwa ya kuzigombanisha Russia na Iran katika kadhia ya Syria. 

Viongozi wa Russia wamezidhihaki njama hizo na kusema kuwa jambo kama hilo haliwezekani kwani Moscow inatambua na kuheshimu manufaa ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Syria.