Iran: Ni kinaya Marekani kuitisha kikao cha IAEA kujadili JCPOA
(last modified Sat, 06 Jul 2019 12:42:19 GMT )
Jul 06, 2019 12:42 UTC
  • Iran: Ni kinaya Marekani kuitisha kikao cha IAEA kujadili JCPOA

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesema ni 'kinaya chungu' kuona Marekani imeitisha mkutano wa dharura wa Bodi ya Magavana ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) kwa lengo la kujadili makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.

Taarifa ya mwakilishi wa kudumu wa Iran katika wakala huo wenye makao makuu yake mjini Vienna imesema kuwa, hatua ya Marekani ya kushinikiza kufanyika mkutano huo wa IAEA inaonesha namna Washington imetengwa kwa kukiuka makubaliano ya pande kadhaa na kuvunja sheria za kimataifa.

Taarifa hiyo imeeleza bayana kuwa, "Ni kinaya chungu kuona Marekani ambayo tayari imejiondoa kwenye JCPOA inaonesha kuwa na wasiwasi wa eti kutotekelezwa vyema makubaliano hayo ya kimataifa. Vitendo vya Donald Trump ndivyo vimeifanya Iran ipunguze kiwango cha kufungamana kwake na makubaliano hayo."

Tehran imesisitiza kuwa, masuala yote yanayohusiana na JCPOA yanayapaswa kujadiliwa na kupatiwa ufumbuzi katika fremu ya mapatano yenyewe.

Yukia Amano, Mkuu wa IAEA ametoa ripoti 15 kuonesha kuwa Iran imefungamana na JCPOA

Mkutano huo wa Bodi ya Magavana wa IAEA unaotazamiwa kufanyika Julai 10 umeshinikizwa na Marekani baada ya Iran kuvuka kiwango cha kilo 300 za akiba ya urani iliyorutubishwa kwa mujibu wa kifungo cha 36 cha JCPOA na kusisitiza kuwa, iwapo pande nyingine za makubaliano hayo hazitatekeleza majukumu yao, Tehran nayo itachukua hatua zaidi.

Licha ya tuhuma zinazotolewa na Marekani kwamba Iran haijatekeleza majukumu wala kuheshimu makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na hata kuituhumu nchi hii kuwa inafanya juhudi za kuunda silaha za nyuklia, lakini ripoti ya Mei 31 ambayo ni mfululizo wa ripoti za Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia (IAEA) ilieleza kuwa, Tehran inaendelea kuheshimu na kutekeleza majukumu yake kuhusiana na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.

Tags