Mahujaji waanza kuelea Mina wakijitayarisha kwa kisimamo cha Arafa
Mahujaji wa Nyumba Tukufu ya Mwenyezi Mungu, al Kaaba leo wameelekea Mina kwa ajili ya kutekeleza ibada ya siku ya Tarwiya hiyo kesho tarehe 8 Dhilhaji katika eneo hilo tukufu.
Njia zote za kuelekea Mina zilijaa mahuhaji kutoka maeneo mbalimbali ya dunia waliokuwa wakitembea kwa miguu huku wakipiga takbira na kumdhukuru Mwenyezi Mungu na maelfu ya wengine walitumia usafiri wa magari kuelekea katika eneo hilo tukufu.
Mahujaji watakesha katika uwanja wa Mina na jioni ya kesho tarehe 8 Dhulhija watafunga safari kuelekea Arafa kwa ajili ya kutekeleza nguzo kuu ya ibada ya Hija tangu alfajiri ya siku ya tarehe 9 Dhilhaji.
Idadi ya mahujaji mwaka huu imetangazwa kuwa ni karibu milioni mbili na nusu wakiwemo milioni 1.8 waliotoka nje ya Saudi Arabia.
Ibada ya Hija inahesabiwa kuwa miongoni mwa mikusanyiko mikubwa zaidi ya kidini duniani.
Mina ni ardhi kubwa iliyoko baina ya silsila ya milima miwili karibu na Mash'arul Haram na mji wa Makka.
Eneo hilo la Mina lina historia ndefu ya kidini na ndipo Nabii Ibrahim (as) alipompiga mawe Shetani na kuchinja mnyama kama fidia badala ya kumchinja mwanaye kipenzi, Ismail (as).