Oct 05, 2019 12:23 UTC
  • UN: Myanmar sio salama kwa Waislamu Warohingya kurejea

Mchunguzi huru wa Umoja wa Mataifa kuhusu Myanmar amesema mamia ya maelfu ya Waislamu wa jamii ya Rohingya waliorejea mkoani Rakhine wakitokea Bangladesh wanakandamizwa na kuandamwa na kila aina ya dhuluma na kwa msingi huo, Myanmar sio salama kwa Warohingya zaidi kurejea.

Yanghee Lee amesema katika ripoti yake iliyokabidhiwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jana Ijumaa kuwa, Waislamu Warohingya huko kaskazini mwa mkoa wa Rakhine wangali wanauawa na kufanyiwa ukandamizaji wa kupindukia, huku wengine wao wakiishi maisha kama ya wafungwa.

Ripota huyo maalumu wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa amesema, "Warohingya hawawezi kuondoka na kutembea huru katika vijiji vyao, jambo ambalo linawafanya waishi kwa kutegemea misaada ya kibinadamu. Kutokana na hali ilivyo, sio salama kwa wakimbizi wa Rohingya kurejea nchini Myanmar."

Wachunguzi wa UN wamekuwa wakisisitiza mara kwa mara kuwa, jeshi la Myanmar lingali linaendeleza mauaji ya kimbari dhidi ya Waislamu Warohingya na kwamba Waislamu hao wanaendelea kukabiliwa na hatari kubwa ya kuangamizwa kizazi chao.

Watoto wa Kirohingya katika maisha ya kutamausha mkoani Rakhine

Ripoti ya jana ya mchunguzi huyo wa Umoja wa Mataifa imebainisha pia kuwa, kitendo cha serikali ya Myanmar cha kuwapa Waislamu Warohingya katika jimbo la Rakhine 'Kadi ya Utambulisho' sio suluhu ya mgogoro wa uraia wa Warohingya, na wanachotaka Waislamu hao ni kupewa uraia kamili, usalama na kurejeshewa ardhi zao walizokuwa wakimiliki kabla ya kuondoka nchini. Serikali ya Myanmar haiwatambui Waislamu Warohingya kuwa ni raia wa nchi hiyo. 

Zaidi ya Waislamu laki sita wa jamii ya Rohingya waliuliwa, laki nane walijeruhiwa na wengine wapatao milioni moja walilazimika kukimbilia nchi jirani ya Bangladesh ili kunusuru maisha yao, baada ya jeshi na Mabudha wenye misimamo ya kufurutu mpaka kuanzisha mauaji ya kinyama Agosti 25 mwaka 2017.

Tags